Makala

AKILIMALI: Vidokezo muhimu vya kukuza na kunufaika na zao la viazi vitamu

July 4th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

VIAZI vitamu ni miongoni mwa vyakula vikuu vya nyumbani na vya kuuzwa nchini Kenya.

Hata hivyo, pato lake linasitishwa na uhaba wa asilia za kupandia.

Hii ni kwa sababu ya kukauka kwa mihimili wakati wa kiangazi na baadhi ya sampuli kuwa na mihimili michache mno.

Viazi vitamu huwa na rangi nyingi kuanzia zambarau, rangi ya chungwa hadi njano au nyeupe.

Kuna tofauti mbalimbali za maumbo, ukubwa, ladha, msokotano, vipindi vya kukomaa na rangi za viazi vitamu kwa ndani. Wakulima wanastahili kutumia sifa hizi kuchagua aina ya viazi vya kupanda.

Teknolojia ya ukuzaji wa haraka wa mimea hii hufanikisha uzalishaji wa viazi vitamu katika kipindi cha kati ya miezi mitatu na sita iwapo itapandwa kwenye mitaro au matuta.

Kwa mujibu wa Bi Scholastic Inyele kutoka kijiji cha Machakha, kata ya Namubila, katika eneo la Sirisia, Bungoma, viazi vitamu hunawiri sana iwapo vitapandwa kwa matuta katika sehemu zinazopata kiasi kikubwa cha mvua katika misimu yote minne ya mwaka.

Zao hili lililo na uwezo wa kuliwa bichi, kuchomwa, kuchemshwa au kuokwa huwa na kiwango kikubwa sana cha madini.

Ni miongoni mwa mazao ambayo huwa rahisi mno kula kwa pamoja na vyakula vya aina mbalimbali. Unapopanda mihimili midogo, panda umbali wa sentimita tano hadi 10 na kina cha sentimita tano.

Iwapo matawi ni mengi kutoka kwa mhimili, yaondoe baadhi yake. Kata na upande katika shamba baada ya kufikia sentimita 30.

Kuotesha viazi vitamu kunahitaji angalau wiki moja au mbili.

Ili kurahisisha hatua hiyo, itakuwa vyema iwapo shamba litaandaliwa mapema na mchanga kupasuliwa na kufanywa nyepesi iwezekanavyo kwenye matuta.

Mkulima anahitajika kutayarisha kitalu cha kupandia viazi vitamu sawia na vile vya karoti au kabeji.

Rotuba

Kama mchanga hauna rotuba ya kutosha, itakulazimu kuongezea mbolea ya samadi.

Mimea ya kupandwa sharti iwe ni yenye nguvu au iliyo na afya na kuwa na sifa zinazohitajika.

Chimba mashimo madogo ya upana wa penseli ili kupanda viazi vitamu kwenye mitaro.

Sentimita 30 na 60 zinastahili kutenganisha shimo moja na jingine.

Iwapo utateua kupanda viazi kwenye matuta, itakujuzu kukata sentimita 30 za miche yenye matawi na majani.

Zamisha kila kipande kwenye dawa ya kopa kwa muda wa dakika 30 ili kuzuia maambukizi ya magonjwa kisha uweke kwenye matuta ambayo yanastahili kuwekwa umbali wa 60×60 shambani.

Bi Inyele anashauri kwamba, wakati mwafaka zaidi wa kupanda viazi vitamu ni katika msimu wa vuli; yaani kipindi cha mvua ndogondogo ambayo huja aghalabu baada ya majira ya baridi. Itakuwa vyema iwapo upanzi wa viazi vitamu utafanywa takriban siku 20 au 30 kabla ya msimu wa masika kuanza.

Kwa kuwa mihimili haina uwezo wa kustawi katika majira ya kiangazi, yastahili ipandwe katika sehemu isiyofikiwa na jua kali au ile inayopokea unyevu na nyuzi joto zisizozidi 18. Viazi vitamu hukuzwa kwa urahisi zaidi katika udongo usio na kiwango cha juu cha asidi (PH 6.3-6.8).