Makala

AKILIMALI: Vifaranga wangu wanakufa ghafla, mbona?

December 13th, 2018 2 min read

SWALI: MIMI ni PHILEMON ETIAT, mfugaji wa kuku wa kienyeji kutoka eneo la Malaba, Busia. Vifaranga wangu wa mwezi mmoja walianza kunyonyoka manyoya na wakaanza kuonekana wanyonge kisha wakaanza kufa ghafla mmoja baada ya mwingine. Je, huu ni ugonjwa gani, na dawa yake ni ipi?

JIBU: MWANZO, kuna sababu tatu kuu zinazosababisha manyoya kumnyonyoka ndege yeyote yule. Ya kwanza ni ile ya kawaida, hasa katika hatua za mwanzoni za ukuaji.

Kunyonyoka huku kwa manyoya ni kwa kifiziolojia na kila ndege hupitia hutua hii. Hali hii pia huambatana na ukosefu wa mwanga wa jua ambao hudhibiti homoni mwilini mwa ndege.

Ndege watapoteza manyoya yao kwa muda fulani kisha yataanza kumea tena baada ya miezi miwili. Ni hali ya kawaida. Lakini ukiwaona vifaranga au kuku wako wakila manyoya yao wenyewe ambayo yashawatoka, hii ni ishara ya ukosefu wa madini muhimu mwilini.

Sababu ya pili ni kuvamiwa na wadudu. Kuna wadudu aina tatu ambao huwasumbua ndege: chawa, siafu na viroboto.

Wadudu hawa wanapomvamia ndege, humlazimisha kujikuna kwa mdomo wake mwenyewe na kujipata amejinyonyoa manyoya kutokana na kule kuwashwa wakati wadudu hawa wanawanyonya damu. Wadudu hawa wasipogunduliwa mapema hutaga mayai ndani ya manyoya na kuenea kwa sehemu nyingi za ndege. Wengine nao hujificha ndani ya magamba kwenye miguu ya ndege.

Suluhu ni kusafisha mazingira ya kuku kisha kuwapa maji yenye kitunguu saumu. Pia washarizie siki ya tufaha (apple vinegar) kwenye manyoya ili kuua chawa na viroboto. Pia unaweza kukausha majani ya mnanaa (mint) na kumwagamwaga kwenye chumba cha kuku.

Ili kutokomeza siafu wanaovamia kuku, changanya vikombe viwili vya maji, kijiko kimoja cha mafuta ya kupikia na kingine cha sabuni ya kuoshea vyombo kisha usharizie chumba cha kuku na kuku wenyewe.

Ya tatu ni ukosefu wa lishe ya kutosha mwilini.

Kuku na vifaranga wake wanapaswa kulishwa vyakula vyenye protini, wanga (carbohydrates) vitamini na madini muhimu.

Manyoya yatanyoyoka kama kuku ana afya duni kutokana na njaa na kiu. Pia kuku huanza kutoa manyoya iwapo kuna joto na msongamano ndani ya chumba ulimowafuga.

Kumbuka mwili wa kifaranga umeundwa kwa asilimia 70 ya maji. Nyuzijoto zikizidi kupanda, maji haya huyeyuka mwilini na kumwacha kifaranga na kiu, hivyo kifo.

Ukosefu wa maji mwilini kwa asilimia 10 utaua vifaranga. Baridi nayo husababisha ugonjwa wa Kichomi (Niumonia) ambao huua vifaranga kwa wingi. Mapafu ya vifaranga waliokufa huwa na rangi isiyokolea ya samawati. Baridi hulazimisha vifaranga kukaribiana ili kupata joto. Msongamano huu huwanyima hewa ya kutosha na baadhi yao hufa. Unashauriwa kuhakikisha nyuzi joto za chumba unamofugia vifaranga ziko kati ya digrii 29 na 35. 3.

Vyakula vyenye sumu inayotokana na vimelea (fungi) au vumbi ya mbao, chumvi nyingi ndani ya maji na gesi hatari (Ammonia, Carbon (I) Oxide na Carbon (II) Oxide) huwaua vifaranga papo hapo.

Kwa kawaida, vifaranga hawana uwezo thabiti mwilini wa kukabiliana na magonjwa. Hivyo, kama usafi haudumishwi, magonjwa kama vile Omphalitis, Pullorum, Salmonellosis na Colibacillosis hukurupuka na kuwaua. (Tutafafanua zaidi kuhusu magonjwa katika makala yajayo.)

-Imekusanywa na CHRIS ADUNGO