Makala

AKILIMALI: Vipodozi vina kazi nyinginezo za taswira na hali mbalimbali

November 14th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

KWA wengi imezoeleka kwamba vipodozi hutumika kumfanya mtu apendeze ama aonekane mwenye umri mdogo zaidi.

Pamoja na dhana hiyo iliyozoeleka, vipodozi pia hutumika kutoa taswira mbalimbali zinazosawiri ama hali chanya au hasi.

Mwanafunzi wa fasheni na urembo na katika chuo cha Ashley’s Hair and Beauty Academy Nairobi, Bi Charity Njoki amekuwa akitumia vipodozi kutoa taswira ya uongo kama vile vidonda vya ajali, vidonda kutokana na risasi au majeraha kama ya mtu aliyekatwa kwa kisu au panga.

Aina hiyo ya vipodozi ijulikanayo kama special effects make-up hutumika sana katika utengenezaji wa filamu.

“Ninaweza kufanya aina mbalimbali ya vipodozi kulingana na sherehe ama wakati tofauti kama vile mchana ama jioni, lakini aina ya special effects make-up bado haijashika kasi hapa nchini,” anasema Bi Njoki.

Bi Charity Njoki. Picha/ Evans Habil

Bi Njoki ambaye ana umri wa miaka 20 anatarajia kuwa kipaji chake cha kutengeneza aina hiyo ya vipodozi itamsaidia kuingia katika sekta ya filamu.

Aina hiyo ya vipodozi pia inajulikana kama SFX make-up.

Wakati wa utengenezaji na uandaaji wa filamu, wahusika hupakwa aina hii ya vipodozi ili kuonyesha majeraha tofauti tofauti.

“Nilipoiweka picha yangu kwenye mtandao nikiwa na aina hii ya vipodozi kwa mara ya kwanza, nilitaka kuwahadaa marafiki zangu kuwa nilikuwa nimehusika katika ajali. Wote waliamini mzaha wangu,” anaeleza Bi Njoki.

Anasema pia yeye hujifunza kutoka kwa mtandao na YouTube na amekuwa akijifunza hatua na utaratibu mpya kila siku.

Azma yake ni kuanzisha duka lake la kusaidia kuendeleza taaluma yake na kuwaajiri watu wengi.

Mpango huu, anasema analenga kuutimiza katika muda wa miaka mitano ijayo.