Makala

AKILIMALI: Wafugaji kuku Kiambu wataka serikali iwapige jeki

July 2nd, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KIKUNDI cha wafugaji wa kuku wapatao 700 kutoka Thika, Kaunti ya Kiambu, kinaendelea kujizatiti licha ya hali ngumu iliyosababishwa  na Covid-19. 

Kikundi hicho kinafuga kuku na kutengeneza pia chakula cha ndege hao eneo la Ngoingwa, Thika.

Msimamizi mkuu wa kikundi hicho Bw Zacharia Munyambu, anasema wanafuga kuku wa kutaga mayai wapatao 800,000 halafu 400,000 ni kuku aina ya broilers, halafu wa kienyeji ni 200,000

Akilimali ilipozuru maskani yao ya kutengeneza chakula cha kuku mnamo Jumanne ilipata ya kwamba wafanyakazi walikuwa wakijitahidi kupakia chakula hicho cha kuku kwa magunia.

Alisema vifaa muhimu vinavyotumika kutegeneza chakula hicho ni mahindi yaliyochanganywa na mbegu za alizeti, mabaki ya ngano, na mchele.

“Kikundi chetu kinapelekea wateja kuku hao na chakula hadi wanakoishi hata wakati huu mgumu wa janga la Covid-19,” anasema Munyambu.

Kikundi hicho kwa niaba ya msimamizi wao huyo kinampongeza mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina kwa kuwafadhili na mtambo wa kutoa vifaranga ambayo inaweza toa vifaranga 1,000 kwa wakati moja.

Bw Wainaina katika mahojiano na waandishi wa habari hivi majuzi alisema wafanyabiashara hasa wa sekta ya juakali wa kiwango cha chini wanastahili kupewa nafasi kuunda bidhaa zao na kutafutiwa soko nchi za nje.

“Hatustahili kutegemea bidhaa kutoka nchi za nje kama China na mataifa mengine. Kwanza tuwape vijana wetu nafasi ya kujiendeleza kupitia juakali,” alinukuliwa akisema.

Ilibainika ya kwamba mwaka 2019 wafugaji wa kuku walipata hasara kubwa baada ya nchi ya China na Uganda kuingiza mayai mengi hapa nchini.

Bw Munyambu anasema vyama vya ushirika vimeinua biashara zao za ufugaji wa kuku.

Wanaitaka serikali izidi kuwainua ili wafanikiwe kwa kuendesha biashara hiyo.