Makala

AKILIMALI: Wana mimea-dawa ya ubora wa juu uliowapa soko Ulaya

January 2nd, 2020 3 min read

Na PETER CHANGTOEK

NI mradi wa jamii ulioasisiwa ili kuikuza mimea kwa mbinu asilia, na kuyasindika mazao na kuyauza katika nchi za nje.

Meru Herbs, ni mradi ambao huikuza mimea mbalimbali, hususan mimea ya viungo vya vyakula, kama vile; mitangawizi na kuboresha thamani ya mazao hayo na kuuza ng’ambo.

Mradi huo uko katika eneo la Tunyai, lililoko katika kaunti ya Tharaka Nithi, na uko katika shamba la ekari tatu, ambalo hutumika kuikuza baadhi ya mimea.

Kwa mujibu Bw Andrew Botta, mshirikishi wa miradi katika taasisi hiyo ni kuwa, asilimia 90 ya bidhaa zao zinazouzwa katika nchi za nje, zimetengenezwa kwa kutumia mazao yaliyozalishwa kwa kutumia mbinu asilia za kilimo.

Miongoni mwa mazao hayo ni: mchaichai au mzumari (lemon grass), majanichai aina ya ‘Hibiscus tea’ na tangawizi. Pia, taasisi hiyo huuza jemu zilizotengenezwa kwa kuyatumia matunda mathalani; maembe, mapapai, malimau, mapera, pamoja na mananasi.

“Sisi huikuza mimea hiyo kwa kuzitumia mbinu za kiasili za kilimo,” afichua Bw Botta.

Taasisi hiyo huikuza baadhi ya mimea wanayoitumia kuzitengeneza bidhaa zao katika shamba lao ambalo ni ekari tatu, na huyanunua mazao mengineyo ya kuyatumia kutoka kwa wakulima waliopewa kandarasi ya kuikuza mimea kwa kuzitumia mbinu asilia za kilimo.

Wao huyanunua matunda kwa Sh25 hadi Sh50 kwa kilo moja, bei za matunda hayo zikitegemea misimu.

Aidha, huyanunua majanichai aina ya ‘hibiscus’ kwa Sh30 kwa kilo moja, ‘chamomile’ kwa Sh60 kwa kilo moja, na michaichai au mizumari (lemon grass) kwa Sh25 kwa kilo.

Baada ya kuvunwa shambani, mavuno hayo huchambuliwa na kuwekwa kwenye gredi mbalimbali na kupimwa uzani, huku usafi wa kiwango cha juu ukidumishwa katika mchakato huo.

“Sisi husindika matunda ili kupata maji au kukata kuwa vipande vidogo, ambapo huweka kwa chupa pamoja na viungo kama vile juisi ya malimau,” aeleza Botta, akiongeza kuwa wao huvikausha viungo na kupakia au kuchanganya na majanichai meusi, ambayo wao huyanunua kutoka kwa kiwanda cha majanichai cha Imenti.

Bidhaa zao huuzwa kupitia kwa jukwaa la ‘Fair Trade’, ambapo bidhaa hizo, huuzwa katika nchi za Japan, Italia, Ufaransa, Austria, Ujerumani, Scotland na Canada.

Mradi huo, awali, uliasisiwa ukiwa mradi wa maji uliokuwa ukinuiwa kuwafaa kwa mafao makubwa wenyeji wa eneo hilo waliokuwa wakikumbwa na ukosefu wa maji.

Awali, mradi huo, ulikuwa ukijulikana kwa jina Ng’uuru Gakirwe Water Project (NGWP), na ulianzishwa na Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Meru, mnamo mwaka 1990; kanisa hilo likishirikiana na serikali ya Italia.

Baada ya kuyapata maji hayo, wenyeji wa eneo hilo wakaanza kuikuza mimea kwa kutumia unyunyiziaji wa maji kwa mimea.

Mwitaliano mmoja aliyekuwa ameishi nchini kwa muda wa miaka mingi, akaanza kuwasihi wakulima kuanza kuukuza mmea aina ya Carcade (Hibiscus sabdariffa), ili wapate riziki kutoka kwa mmea wenyewe.

Wakulima walioitikia wito huo, walikuwa 430.

“Ukuzaji wa Carcade ukawa ndio mwanzo wa ‘Meru Herbs’. Tulianzisha taasisi hii kama chama cha ushirika cha wanachama wa mradi wa unyunyiziaji maji mashamba, mnamo mwaka 1991,” afichua Botta.

Baadaye, wanachama wakakianzisha chama cha ushirika na mkopo (Sacco) ili wanachama wakitumie kuweka akiba ya fedha, na kupata mikopo itozwayo riba ya chini.

“Japo sisi hupata mazao hapa karibu, baadhi ya bidhaa hutolewa nje ya Kenya. Kwa mfano, majagi ya kupakia huagizwa kutoka Misri, vifuniko hutoka Afrika Kusini, na mifuko ya kupakia majanichai hutoka Ufaransa,” adokeza Botta, akisisitiza kwamba, ni sharti kuwe na idhini, ili waziuze bidhaa zao nje ya

nchi.

Kwa mujibu wa mshirikishi huyo wa miradi, mazao yao huzalishwa bila kutumia mbolea za kemikali au viuadudu (pesticides) vyenye kemikali.

“Kilimohai pia hutunza mazingira,” asema.

Wao wana kibali cha kimataifa kutoka kwa Ecocert- shirika lililoko nchini Ufaransa, na wanaendelea kutafuta idhini kutoka kwa mataifa mengineyo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Meru Herbs, Sally Sawaya, siri ya kufanikiwa katika shughuli ya kuziuza bidhaa zao katika mataifa ya nje ni kuyazalisha mazao yenye kiwango cha juu cha ubora.

Sawaya anasema kuwa wateja wengi humu nchini hudhani kuwa mazao yaliyozalishwa kwa mbinu asilia za kilimo ni za hali ya juu, na ni ghali mno.

Hata hivyo, anaongeza kuwa wanajaribu pia kuziuza bidhaa zao kwa wingi nchini.

Wao hushirikiana na wakulima ambao wamepewa kandarasi ya kuikuza mimea mbalimbali kwa kuzitumia mbinu faafu za kilimo, pasi na kuzitumia kemikali katika uzalishaji wa mazao.

Pindi tu mazao yanapokuwa tayari, wakulima hao huyawasilisha mazao hayo katika Meru Herbs, ambapo hutumika kuzitengeneza bidhaa aina ainati.