Makala

AKILIMALI: Wateja hufuata mpunga wake wa pishori shambani

February 28th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANANCHI wana mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inakua. Ili kuhakikisha kwamba ruwaza ya mwaka wa 2030 inafikiwa, wakulima wanahitaji kuungwa mkono ndipo wazalishe chakula cha kutosha nchini.

Uchumi katika kaunti ya Kirinyaga unategemea sekta ya kilimo kwa kiasi kikubwa. Katika kaunti ndogo ya Mwea kwa mfano, kilimo kinachofanyika kwa wingi zaidi ni kile cha mpunga ambao huzalisha mchele.

Akilimali ilikutana na Bw Simon Njagi Gichovi katika eneo la Nyangati, Mwea wiki jana. Anasema amekuwa akishiriki kilimo cha mchele kutoka mwaka wa 2000.

Bw Njagi anajihusisha si tu na kilimo cha mchele peke yake, bali pia anakuza ndizi, miwa na viazi. Kwa minajili ya kilimo cha mchele haswa, ametenga sehemu ya ekari moja na nusu katika shamba lake.

Bw Simon Njagi Gichovi katika shamba la mpunga analolimiliki katika eneo la Nyangati, Mwea, Kaunti ya Kirinyaga. Picha/ Chris Adungo

Kwa kawaida, yeye hukuza mchele aina ya pishori ambao hupandwa kwa misimu miwili kila mwaka.

Kulingana naye, msimu wa kwanza huanza katika mwezi wa tisa hadi wa kumi na mbili na kisha baadaye msimu wa pili kuanza Januari hadi Aprili.

Bw Njagi huwa anaandaa mbegu za mchele katika sehemu teule ili kuziwezesha kukua hadi kufikia urefu wa miche ambayo huchukuwa muda wa kati ya wiki mbili na wiki tatu kabla ya kuhamishwa na kupandwa katika sehemu zingine za shamba kubwa alilokwisha kuliandaa kwa ajili ya upanzi.

“Kwa muda wa wiki moja baada ya upanzi, huwa nawekea mimea hii mbolea aina ya DAP ili kuwezesha mpunga kukua kwa njia bora na baadaye katika wiki ya tatu, huwa napalilia kwa kung’oa, magugu, majani na mimea mingine isiyohitajika shambani,” akaelezea Bw Njagi.

Katika muda huu wote, huwa anahakikisha kwamba mpunga umepata maji kwa wingi kwani ni njia mojawapo ya kuuwezesha kunawiri vyema.

Baada ya miezi miwili, mpunga huanza kutoa maua na wakati huu, Bw Njagi huwa analazimika kuwaajiri wafanyakazi wa kumsadia kuwawinga ndege ambao mara nyingi huvamia mmea huu na kula mazao ya mpunga.

Njagi anasema kuwa mpunga unapofikisha miezi minne shambani, huwa tayari umeanza kukomaa na wakati huu maji yanayoingia shambani hupunguzwa ili kuupa nafasi nzuri ya kukauka ipasavyo.

Mwishoni mwa mwezi huu wa nne, shughuli inayofanyika ni kukata mimea hii kote shambani kama hatua ya kwanza ya kuanza kuvuna.

Kwa mara nyingi, msimu wa mavuno unapokamilika, Njagi hupata takriban magunia 30 ya mchele katika msimu wa kwanza.
Soko la bidhaa hili muhimu ni kwa watu binafsi na wafanyabiashara ambao wengi wao hujia mazao haya shambani mwa Bw Njau.

Katika msimu, mzuri bei ya kilo moja ya mchele huu wa pishori huuzwa kwa kati ya Sh60 na Sh65.

Baada ya shughuli hizi zote, huwa anaanza upanzi tena mnamo Januari tayari kwa msimu wa pili. Msimu huu wa pili huendelea hadi mwezi wa nne.

Changamoto zipo

Baadhi ya changamoto anazozipitia kwa wingi ni makadirio ya mara kwa mara ya hasara kubwa kutokana na ndege ambao hula mchele unapochipuka kabla ya kukomaa.

Pia ukosefu wa maji katika misimu ya kiangazi ni changamoto ambayo hutishia kukilemaza kilimo chake.

Bw Njagi anasema kuwa bei ghali ya mbolea na hela nyingi zinazotumika katika kulipa wafanyakazi nyakati ambazo ndege wanahatarisha mazao ya mchele, hutatiza wakulima wengi.

Mwito wake kwa wakulima wengine ni waweze kujihusisha na kilimo hiki cha mchele na bila shaka watafanikiwa kimapato.

Pia anawashauri vijana wenye nguvu na maarifa mengi ya kisasa kwamba wanapaswa kuhusika na kilimo hiki na waweze kukiboresha zaidi.

Ombi lake kwa serikali ya Kaunti ya Kirinyaga pamoja na serikali kuu ni kuwepo kwa uhakika kwamba wakulima wanapata mbegu bora na elimu kuhusu namna ya kuendesha ukulima huu kwa njia za kisasa zaidi.

Ili kufanikisha haya, maonyesho ya kilimo na semina kuhusu kilimo zinapaswa kufanyika maa kwa mara kwa njia zinazowashirikisha wakulima zaidi.