Makala

AKILIMALI: Weledi wa chipukizi wa 4K Club katika kilimo hutia wengi shime

June 13th, 2019 2 min read

Na STANLEY KIMUGE na CHARLES WASONGA

KILA Jumatatu na Ijumaa, Jabez Kipchumba, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 13 hushirikiana na wenzake katika Shule ya Msingi ya Gethsemane Christian Academy kufanya kazi mbalimbali katika shamba la shule hiyo.

Kwa muda wa saa moja wanafunzi wa shule hiyo iliyoko mjini Eldoret hutunza mazao mbalimbali kama vile mboga za aina ya sukuma wiki, spinachi, nyanya, vitunguu, pilipili hoho, tango (cucumber) na mboga za kienyeji kama managu.

Siku hizi huwa zimetengewa wanachama wa chama cha kilimo, almaarufu 4K Club, ambao wako katika madarasa ya tano, sita na saba, kujifunza shughuli mbalimbali kama, kupalilia mimea shambani, kupanda miche ya miti, kuvuna mazao na kukamua ng’ombe.

Mazao hayo ya shambani hupikiwa wanafunzi shuleni humo huku mengine yakiuzwa kwa wafanyabiashara na watu binafsi.

Kilo moja ya sukuma wiki huuzwa kwa Sh30 kulingana na msimu. Lakini managu huuzwa kwa Sh80 na zaidi kwa kilo.

“Tumefunzwa mbinu za kutunza mimea mbalimbali kando na kukabili magonjwa na wadudu waharibifu. Kwa mfano tumefunzwa namna ya kuangamiza wadudu kama cutworms na aphids ambao huathiri mimea na kuigeuza kuwa manjano. Hutoboa mashimo kwenye matawi ya sukumawiki,” Kipchumba anaeleza.

Shamba hilo liko kando ya Mto Marura, chanzo cha maji ambayo hupigwa kwa kutumia jenereta na kutumiwa kunyunyizia mimea.

Mwalimu John Odhiambo, ambaye ni msimamizi mkuu wa 4K Club anasema shule hiyo ilifufua klabu hiyo mwaka jana kwa kusajili wanachama 15. Idadi ya wanachama sasa imepanda hadi 38.

Katika shamba hilo la ukubwa wa ekari moja, kuna vitalu vitatu vya miche ya aina mbalimbali ya miti. Miche hiyo huuzwa kwa wateja kutoka nje kwa kati ya Sh10 hadi Sh100 kulingana na aina ya miche.

“Miche ya mboga nayo hukaa kwenye vitalu kwa muda wa majuma mawili kabla ya kupandwa shambani,” anasema Bw Odhiambo.

Kipchumba, mwanafunzi wa Darasa la Saba, ambaye pia ndiye kiongozi wa 4K Club anasema yeye hupanda sukumawiki na nyanya nyumbani kwao kwa kutumia ujuzi na maarifa aliyopata shuleni.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Gethsemane Christian Academy ambao ni wanachama wa 4K Club wakiendesha shughuli ya utunzaji mboga katika shamba la shule yao. Picha/ Stanley Kimuge

“Mboga niliyopanda nyuma ya nyumba yetu hutusaidia kwa matumizi ya nyumbani. Kwa hivyo mama huwa hasumbuki kwenda kununua mboga na nyanya sokoni,” anasema.

Naye Redempta Jeruto,11, anasema: “Kilimo ni kazi nzuri ambayo inafurahisha. Mimi hupendezwa na vitunguu pamoja na nyanya.”

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ibrahim Esitoko anasema kauli mbiu ya 4K Club ni, “You learn by doing” (Unajifunza kwa kufanya) ambayo huwasaidia wanafunzi kutenda yale waliojifunza katika hali halisi manyumbani mwao.

“Tuligundua kwamba ni muhimu kuwafunza wanafunzi wetu fani mbalimbali za kilimo. Kwa kuwa nafasi za ajira ya ofisi nyakati hizi ni chache mno, watang’amua kuwa wanaweza kutengeneza pesa kupitia kilimo,” anasema Esitoko huku akiongeza kuwa wafanyakazi watatu wameajiriwa katika shamba hilo kuendesha mradi huo.

Mojawapo ya changamoto inayowakumba ni mafuriko ambayo husomba mimea mvua inaponyesha kwa wingi.

Shule hii pia inafuga ng’ombe wa maziwa aina Jersey, Friesian na Ayrshire. Wakati huu wana jumla ya ng’ombe 12, sita kati yao huzalisha jumla ya lita 60 za maziwa kila siku.

“Friesian ambaye hutupa faida kubwa huzalisha lita 29 ya maziwa kila siku,” anasema Esitoko.

Kimsingi, anaongeza, shule huchuma Sh360,000 kutokana na mauzo ya mboga na Sh192,000 kutokana na mauzo ya maziwa kila mwaka.

Shule hiyo pia hutengeneza mbolea ya kiasili kwa kutumia samadi kutoka kwa ng’ombe hao na mabaki ya mimea shambani.

Waziri wa Kilimo katika kaunti ya Uasin Gishu Bw Samuel Yego anapongeza mradi kama huo akitoa wito kwa shule zingine katika kaunti hiyo kuiga mfano huo.

“Mradi kama huu utawafanya vijana wetu kutambua umuhimu wa kilimo. Unaondoa dhana potovu miongoni mwa kizazi cha sasa kwamba shughuli za kilimo hazina mapato ya juu. Natoa wito kwa watoto waige hawa wa Shule ya Gethsemane Christian Academy ili kuimarisha mapato katika familia zao,” anasema Waziri Yego.