Makala

AKILIMALI: Wizi wa mifugo ulimfanya aingilie kilimo; sasa hajuti

October 10th, 2019 3 min read

Na SAMUEL BAYA

MWAKA wa 2009 wakati wa kilele cha wizi wa mifugo kati ya jamii za Wasamburu, Wapokoti na Waturkana, Mathew Lesiyampe alikuwa mmoja wa wahasiriwa.

Kwa sababu alikuwa mfugaji, boma lake lilivamiwa usiku mmoja na wezi wa mifugo na kutoroka na ng’ombe 40 wenye thamani ya Sh1 milioni.

Ingawa aliponea kifo katika uvamizi huo katika kijiji cha kwao cha Lolkunono katika wadi ya Loosuk, hakuwahi kuwapata tena mifugo wake.

Alisema katika mahojiano yetu mjini Maralal majuzi kwamba baada ya wizi huo kutulia, zaidi ya watu 60 walikuwa wamepoteza maisha yao huku mifugo zaidi ya 3,000 ikiibiwa na majangili.

“Nashukuru Mungu kwamba niliponea lakini mifugo wangu 40 waliangamia. Tukio hilo hata hivyo lilinifanya nianze kufikiria upya kuhusu mtazamo wangu wa kufuga mifugo,” akaambia Akilimali.

Uvamizi huo ulimfanya Lesiyampe kuondoka kijijini na kuelekea mjini Maralal, ambako akiwa hapo aliamua kuchukua mkopo wa Sh3 millioni kutoka kwa benki moja ili kuanza shughuli za kilimo.

“Kulingana na yale ambayo nilishuhudia, niliondoka eneo la Loosuk na kuamua kwenda kuishi mjini Maralal. Sikuwa tayari tena kuingilia masuala ya mifugo kwa sababu sekta hiyo ndiyo ambayo iko na vita vikali vya wizi kila mara,” akasema. Alipochukua mkopo huo mwaka wa 2010, aliamua kurudi kijijini lakini mara hii akiwa tayari kuanza ukuzaji wa mboga katika kipande cha ekari tatu ambacho alikuwa amenunua.

“Nikiwa na pesa hizo, niliamua kununua ekari tatu, nikachimba kisima na kuanza kukuza mboga.

“Ni miaka kumi baadaye na sasa mimi ni miongoni mwa wakulima wa mboga ambao wako na soko kubwa la biashara hii katika Kaunti ya Samburu na kaunti nyengine jirani,” akasema.

Alianza kwa kupanda kabeji 9,000 ambazo aliuza kwa bei ya Sh100 kwa moja baada ya miezi mitatu na kupata Sh900,000.

“Hii ilikuwa pesa nyingi sana kwa mwanzo wowote ule wa biashara na sijarudi nyuma tena,” akasema Lesiyampe.

Miezi mitatu baada ya kuvuna mboga zake za kwanza, aliongeza tena kabeji zingine na kuwa na kabeji 20,000.

Alipouza mboga hizo kwa Sh100 kwa kabeji moja aliweza kuvuna Sh2 milioni.

“Ndani ya mwaka mmoja, nilikuwa nimelipa mkopo wangu wa Sh3 milioni ambao nilikuwa nimekopa baada ya biashara hii ya mboga kuimarika maradufu,” akasema.

Kwa hivi sasa, Lesiyampe anauza nyanya, kabeji na biringanya kwa shule na, vyuo vikuu. Vile vile, yeye ameibuka miongoni mwa wakulima ambao wana soko kubwa la mboga katika mji wa Nyahururu, Rumuruti na hata Nakuru.

“Niliamua kuajiri meneja wa shamba ambaye ana ufahamu na masuala ya ukulima. Kwa sababu ya bidii yangu, sasa nimeweza kuimarisha maisha yangu kupitia kwa kilimo hiki, hasa katika kaunti ambayo watu wengi walidhania ni kame na hakuna kilimo chochote kinachoweza kuendelea hapa,” akasema.

Kupitia kuimarika kwa shamba lake, Lesiyampe na meneja wake waliamua kuligawanya mara tatu, huku kila ekari ikitumika kukuza kila aina fulani ya mboga.

Kwa sasa mkulima huyu ameajiri akina mama kumi ambao wanafanya kazi kama vibarua katika shamba lake huku kila mmoja akilipwa ujira wa Sh500 kwa siku.

“Hiyo ina maana kwamba ninalipa Sh5,000 kwa siku na hawa akina mama wakifanya kazi kwa siku mbili, mimi huwalipa Sh10,000. Kazi yao kubwa ni kulima na kuondoa kwekwe ambayo huwa inaharibu mimea yangu,” akasema.

Aliongeza kwamba hutumia Sh50,000 kukodisha malori matano kupeleka mazao yake sokoni na kwa mwezi gharama ya kilimo hufikia kiasi cha Sh200,000.

Hata hivyo alisema anahesabu faida kwa sababu gharama hiyo inamletea Sh2 milioni. Vilevile amenunua ardhi kubwa zaidi kwa lengo la kupanua biashara yake na sehemu ya ardhi hiyo amewapatia akina mama ambao wameamua kujihusisha na ukulima kama njia ya kujipatia riziki.

“Mimi ni baba ya watoto wanne, wasichana watatu na mvulana mmoja. Binti yangu alikamilisha elimu ya shahada ya kwanza ya chuo kikuu na sasa anasomea shahada ya uzamili. Wote wamesoma vizuri kupitia kilimo hiki. Ninaamini kwamba Kaunti ya Samburu bado ni eneo ambalo ni bora katika kilimo na linaloweza kulisha hata kaunti zingine. Ni wakati sasa watu waamke na waone picha tofauti kuhusu kaunti hii. Huu ufugaji wa mifugo hauwezi kutusaidia sana kupambana na dhiki za njaa na umaskini,” akasema Lesiyampe.

Ni kauli iliyoungwa mkono na mkurugenzi wa kilimo katika kaunti ya Samburu, Tyson Lemako ambaye alisema kuwa kaunti imejitolea mhanga kuhakikisha kwamba kilimo sasa kinaanza kuwa uti wa mgongo kwa wakazi wa eneo hilo.