Akina mama wasababisha msongamano Nakuru wakisherehekea kuteuliwa kwa Karua

Akina mama wasababisha msongamano Nakuru wakisherehekea kuteuliwa kwa Karua

NA RICHARD MAOSI

BAADHI ya akina mama kutoka kaunti ya Nakuru wamesherehekea katika barabara ya Kenyatta ikiwa siku moja baada ya kinara wa Azimio La Umoja Raila Odinga, kumtangaza Bi Martha Karua awe mgombea mwenza wake.

Wakiongozwa na Bi Jedidiah Kiplenge ambaye atawania kiti cha ubunge eneo la Nakuru Magharibi, walitumia barabara ya Kenyatta na kusababisha msongamano mkubwa wa magari, huku waendeshaji pikipiki na magari wakilazimika kusitisha safari zao kwa muda.

“Hii ni fahari kubwa kwa wanawake wa nchi hii, ndio sababu kwa kauli moja tumeamua kuunga mkono Raila Odinga kuwa rais wa tano wa nchi hii,” akasema Jedidiah.

Jedidiah alieleza Taifa Leo kuwa Odinga ameonyesha imani yake kwa akina mama ambao wanachukua idadi kubwa ya wapigaji kura waliosajiliwa ya asilimia 51.

Alisema kuwa akina mama kutoka kote nchini wameungana ili kuhakikisha mgombea huyo wa urais anaingia ikulu ifikapo Agosti 9, 2022 baada ya uchaguzi mkuu.

Naye Bi Monica Moraa ambaye ni mchuuzi wa matunda katika soko la Top Market Nakuru alisema Bi Karua amekuwa akitetea wanawake.

Moraa aliongezea kuwa Kenya inahitaji viongozi wakakamavu na wenye msimamo thabiti kama Karua ambao hawawezi kuyumbishwa na dhoruba kali la kisiasa.

Kulingana na Moraa huu ni mwamko mpya kwani taifa halijawahi kupata kiongozi mwanamke kuchukua wadhifa wa naibu rais tangu taifa lipate uhuru mwaka 1963.

Baadhi ya wanawake ambao wamejaribu kugombea urais katika siku za awali ni kama Bi Charity Ngilu na Martha Karua, lakini hawakufua dafu.

  • Tags

You can share this post!

Rigathi Gachagua aahidi kuwaambia wakazi wa Mathira...

Kipa mdogo kiumri mwenye uzoefu langoni

T L