Akinyi na Kangangi wachupa uongozoni mbio za baiskeli za Migration Gravel Race

Akinyi na Kangangi wachupa uongozoni mbio za baiskeli za Migration Gravel Race

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Nancy Akinyi na Suleiman Kangangi walitamba katika siku ya pili ya mbio za kimataifa za baiskeli za Migration Gravel Race (MGR) katika hifadhi ya Maasai Mara kaunti ya Narok, Juni 19.

Mwamerika Lael Wilcox na Mkenya John Kariuki walikuwa washindi wa mkondo wa kwanza ulianzia kituo cha mafunzo cha Mara (MTC) hadi kambi ya Majimoto mnamo Juni 18 ukijumuisha kilomita 128.

Akinyi, ambaye ni bingwa mtetezi wa mbio hizo za kilomita 650 zilizoanzishwa mwaka 2021, alirukia nafasi ya kwanza kutoka nafasi ya tatu siku ya kwanza katika mkondo wa pili ulioanzia Majimoto hadi Marijo ukijumuisha kilomita 172. Alifuatiwa na Xaverine Nirere kutoka Rwanda na Lael mtawalia.

Kangangi, ambaye alikuwa na siku mbaya Juni 18 baada ya baiskeli yake kukumbwa na matatizo ya kiufundi kilomita tano pekee ndani ya mashindano, alitetemesha katika mkondo wa pili. Baiskeli ya Kangangi ilirekebishwa siku ya kwanza na alijitahidi akamaliza mkondo huo, japo akiwa amechelewa sana.

Siku ya pili, Mwitaliano Mattia de Marchi, ambaye alikamata nafasi ya pili katika mkondo wa kwanza, alionekana kuelekea kutawala pia mkondo wa pili baada ya kufungua mwanya wa karibu kilomita moja. Hata hivyo, Kangangi alijikakamua na kumuonyesha Marchi kivumbi katika kupanda milima. Marchi aliibuka nambari mbili naye Kariuki akafunga tatu-bora. Mkenya Geoffrey Lang’at alipata ajali na kusafirishwa hadi jijini Nairobi kupokea matibabu.

Mashindano hayo yataingia siku ya tatu Juni 20 ambapo waendeshaji hao wa baiskeli watafanya kilomita 129 kati ya eneo la Marijo na Aitong. Mashindano yatakamilika Juni 21 wakati washiriki wataendesha basikeli zao kilomita 164 kutoka Aitong hadi MTC. Waendeshaji 95 wa baiskeli kutoka mataifa 15 walianza mashindano hayo. Washiriki wamepata kuona nyumbu, mbuni, swara, pundamilia, twiga na kongoni katika mbuga ya Masai Mara.

  • Tags

You can share this post!

Sadio Mane aendea mamilioni ya Bayern Munich

Chama cha UDA chataka Babu Owino azimwe kushiriki uchaguzi...

T L