Dondoo

Akiona kufurahisha kipusa kwa ujira wa watu

July 5th, 2019 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

KABOROK, KERICHO

FUNDI wa eneo hili alijipata kona mbaya alipokabiliwa na vibarua kwa kutumia pesa kumfurahisha kipusa badala ya kuwalipa.

Meza ya dondoo iliarifiwa kuwa mdosi alimpa fundi huyo kazi kumjengea nyumba ya kisasa naye akaawajiri vibarua kumsaidia.

“Mwanzoni, fundi alikuwa akiwalipa vibarua kila siku pesa zao kwa kumwaga jasho katika mjengo. Hata hivyo, alianza kukosa kuwalipa na kuwaahidi kuwa angewalipa donge kwa kazi ya siku kadhaa,” mdokezi alisimulia.

Vibarua walivumilia kwa siku chache kabla ya kuzusha vikali na fundi akajaribu kuwatuliza.

“Msiwe na wasiwasi hata kidogo. Mdosi amedinda kunilipa hadi kazi isonge mbele kabisa. Mtwange tu kazi mkijua mtapata donge akitoa pesa,” fundi aliwabembeleza vijana hao.

Walipolia hawakuwa na pesa za kununua chakula, fundi aliwashauri wakope katika maduka tofauti wakiahidi kulipa wakipata hela.

“Usipotulipa mwishoni mwa wiki hii utaona cha mtema kuni. Hauwezi kutufanya watumwa hapa huku watoto wetu wakikesha njaa,” mmoja wa vibarua alimtisha fundi naye akacheka na kudai kila mmoja wao angepata haki yake bila shaka.

Juzi, mdosi alifika kukagua mjengo huo. Baada ya kutembea hapa na pale, aliwataka wajenzi wafanye hima.

“Ninataka muache uzembe na mnifanyie kazi hima maana nimekuwa nikitoa pesa kila siku ili msifike nyumbani mikono mitupu,” mdosi alizusha. Mara moja, mafundi hao walimkabili mkubwa wao na kumtia adhabu kwa makofi na mateke.

” Kumbe hela zetu zimeliwa na hawara wako,” mmoja wao alisema akimtwanga kwa ngumi. Mwenye kazi aliwatuliza barobaro hao na akaahidi kuwa akiwalipa moja kwa moja.