Habari

Aelezea sababu ya kujifanya muuguzi wa kike tangu 2009

June 20th, 2019 1 min read

Na TITUS OMINDE

MWANAMUME ambaye alikamatwa maajuzi katika hospitali ya Moi Teaching and Referral akijifanya muuguzi wa kike, amekiri amekuwa akijifanya mwanamke tangu 2009.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, mwanamume huyo alikiri kuwa yeye ni mwanaume wala hana maumbile yoyote ya kike.

Alieleza kuwa alianza tabia hiyo mnamo 2009 baada ya kukamilisha masomo katika shule ya msingi ya Muget, ambako alifanya mtihani wa KCPE.

Mwanaume huyo ni mzaliwa wa kijiji cha Kapchekenya, kaunti ndogo ya Moiben, Uasin Gishu.

Licha ya kijifanya mwanamke alisema alitahiriwa mwaka huo wa 2009 kwa mujibu wa mila za jamii ya Wakalenjin.

Mbali na kushiriki mashindano ya riadha kama mwanamke, alisema amewahi kufanya kazi ya uyaya mjini Mombasa katika mtaa wa Mikindani.

“Tangu nianze kujifanya mwanamke nimefanya kazi mbalimbali kama mwanamke ikiwa ni pamoja na uyaya, ambapo nilikuwa nikifanya kazi ya nyumbani katika nyumba ya mama mmoja muuguzi eneo la Mikindani mjini Mombasa mnamo 2014,” alisema Hillary Kiprotich, ambaye amekuwa akijitambulisha kwa jina la kike la Shieys Chepkosgei.

Kusaka riziki

Mwanaume huyo alisema aliamua kujifanya mwanamke kama njia moja ya kujipatia riziki kwa urahisi badala ya kung’ang’ana na wanaume wenzake.

“Tangu utoto nilipenda tu kuwa mwanamke hasa kwa kushiriki maisha yangu na wasichana wadogo. Michezo ya utoto nilicheza na wasichana,” alisema

Vile vile amekuwa akishiriki mashindano ya mbio kwa kushindana na wasichana kwa manufaa yake mwenyewe.

Miongoni mwa mbio ambazo ameshiriki kama mwanamke ni mbio za kimataifa nchini Afrika Kusini 2014, Malaysia 2015 na Zambia miongoni mwa mataifa mengine

Hata hivyo alipigwa marufuku kushiriki mbio baada ya kupatikana akitumia dawa za kusisimua misuli mnamo 2016.

Mapema wiki hii alishtakiwa katika mahakama mjini Elodret kwa kujifanya muuguzi wa kike katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi MTRH mjini Eldoret.

Kesi hiyo ilichukua mkondo mpya baada ya maafisa wa gereza la wanawake kumrejesha mahakamani wakidai kuwa hakuwa mwanamke kama ilivyodaiwa.