Akita kwa kilimo mseto baada ya kuacha ualimu

Akita kwa kilimo mseto baada ya kuacha ualimu

NA PETER CHANGTOEK

UGONJWA wa Covid-19 ulipoingia nchini, watu wengi walitafuta njia mbadala za kujipatia riziki.

Margaret Njenga ni mmojawapo wa wale waliotafuta njia mbadala za kujiruzuku, baada ya taasisi za elimu kufungwa na serikali, kama njia ya kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo hatari.

Alikuwa mwalimu wa shule moja ya msingi. Hata hivyo, alipogundua kuwa kuna faida katika kilimo, akaamua kutorudi darasani.

“Nilikuwa nimefunza kwa muda wa miaka minne tu, kabla ugonjwa haujaingia. Shule zilipofungwa, nikaja hapa kuendeleza kilimo. Baba yangu alikuwa akiikuza mimea ya mahindi na maharagwe hapa. Kuanzia Machi hadi Disemba 2020, niligundua kuwa kuna faida kwa kilimo, nikaamua kuwa sitarudi tena kufunza,” aeleza Margaret, ambaye alisomea taaluma ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha St John’s, Kilimambogo.

Kwa sasa, ni mkulima hodari anayeikuza mimea mbalimbali, kama vile vitunguu, pilipili mboga, bitiruti, kabichi, spinachi, sukumawiki, nyanya, miongoni mwa mingine.

Aidha, huwafuga ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kuku, bata na sungura.Anasema kuwa, alilazimika kulitayarisha shamba vizuri kwanza, kwa kuweka mifereji ya kunyunyizia maji kwa sababu eneo hilo hukumbwa na kiangazi.

“Katika shamba la nusu ekari, nilitumia Sh200,000 kuweka paipu, kwa nguvukazi na kununua vitu vya kutumia shambani. Katika shamba lile jingine la nusu ekari ambalo limekuwa na vitunguu, nilitumia Sh270,000, kwa sababu lina paipu nne,” asema mkulima huyo, ambaye alikuwa amevuna vitunguu vingi Akilimali ilipowasili shambani.

Anafichua kuwa, vitunguu huchukua muda wa siku 45 kwenye kitalu, na siku 90 kwa shamba baada ya kupandikizwa.

Nayo mimea ya sukumawiki na kabichi huchukua muda wa siku 21 kwa kitalu na miezi mitatu baada ya kupandikizwa na kupandwa shambani.

Mkulima huyo, mwenye umri wa miaka 35, ana kivungulio kidogo, ambacho hukitumia kuziotesha mbegu za mimea yake kwa trei spesheli.

“Mimi sinunui miche, huikuza,” asema, akisisitiza kuwa, huvipenda vitunguu mno, kwa kuwa ndivyo humpa fedha nyingi.

Kwa mujibu wa Margaret ni kuwa, kabichi, sukumawiki na mimea mingineyo, humsaidia kupata fedha za kujiendeleza na hata kuwalipa wafanyakazi, anaposubiri kupata donge nono kutoka kwa vitunguu.

Hata hivyo, anadokeza kuwa, kuna wakati ambapo bei ya vitunguu ilikuwa chini mno, na alishurutika kuuza kilo moja kwa Sh30.

“Ilipanda ikawa Sh50, Sh60, na kwa sasa, ninauza kwa Sh70 kwa kilo,” aongeza.

Anasema kuwa, ili kufanikiwa katika kilimo, mkulima anafaa kuikuza mimea kwa wingi. Anaongeza kwamba, mkulima akiwa na tani nyingi za mazao, mapato yatakuwa mengi.

Akivuna vitunguu katika sehemu moja ya shamba, huipanda mimea tofauti tofauti, kama vile kabichi au nyanya, katika sehemu hiyo.

“Manufaa ya kufanya kilimo mseto ni kuwa, hutakosa pesa mfukoni. Kwangu, vitunguu huchukua muda mrefu; kwa hivyo, ninapongojea vitunguu, huuza kabichi na nyanya,” asema, akiongeza kuwa, kwa kufanya hivyo, gharama ya uzalishaji huwa chini.

Mkulima huyo hutumia mbolea asilia za mifugo kutoka kwa shamba lake kuikuza mimea.

Pia, hununua mbolea kutoka kwa majirani.

Margaret anasema kwamba, kabla mkulima hajajitosa katika ukuzaji wa mimea, anafaa kuhakikisha kwamba udongo anaonuia kuutumia kwa ukuzaji wa mimea, unafaa kupimwa ili kujua ni virutubisho gani vinavyohitajika shambani.

Mkulima huyo anasema kwamba, kunapokuwa na joto jingi, hunyunyizia maji kwa muda wa dakika 30, jioni.

Mbali na mimea, kwa wakati huu, ana kuku 70; wa kienyeji na gredi. Anasema kuwa, huwanunua vifaranga wenye umri wa siku moja, na kuwauza baada ya mwezi mmoja.

“Mwezi uliopita, niliwanunua 100, nikawauza 60 nikabaki na 40. Huwanunua kwa Sh100 na kuwauza kwa Sh400 baada ya mwezi mmoja. Huuza jogoo wa kienyeji kwa Sh1,500 na wa kike kwa Sh800,” asema, akiongeza kuwa, huuza yai kwa Sh20.

Huyauza maziwa lita 70 kwa shirika moja lililoko katika eneo la Kiserian, kwa bei ya Sh40 kwa lita moja. Huyauza maziwa hayo mara mbili kwa siku; asubuhi na adh huri.

Mkulima huyo, ambaye pia ana mbuzi na sungura kadhaa, anasema kuwa, ana mipango ya kuongeza thamani kwa mazao ya nyanya na vitunguu.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Wadumisha soko la maua ya waridi

Karua apiga jeki wawaniaji wa kike – Utafiti

T L