Dondoo

Akosoa shemeji kwa ‘kumharibia’ mke

October 8th, 2020 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

RUNDA, Nairobi

BUDA wa eneo hili alikasirika na kutishia kumtimua shemeji yake kwake akimlaumu kwa kumpotosha mkewe.

Mwanadada huyo alikuwa ameishi kwa buda kwa miezi sita madai hayo yalipoibuka.

“Wewe nimekutazama siku nyingi sana na sasa nimechoka. Hata kama mke wangu ni dada yako achana naye kabisa,” buda alimuonya.

Kulingana na mdokezi, buda alidai kwamba mwanadada alikuwa na tabia mbaya aliyokuwa amemwambukiza mkewe.

“Wewe ni shemeji yangu lakini tabia zako si nzuri. Tangu uje hapa mke wangu amekuwa na madharau mengi sana kwangu na jamaa zangu,” alimfokea kidosho.

Duru zinasema kidosho alibaki mdomo wazi asijue namna ya kujitetea.

“Mambo yako nayajua sana. Hata ile siku ulikuja hapa nilikuwa na wasiwasi sana,” buda alimkaripia kidosho.

“Nilishangaa sana juzi mke wangu akiniambia mimi ni mzembe na kazi kitandani siwezi,” jamaa alisema huku hasira zikimpanda.

Inadaiwa mkewe alijaribu kumtuliza lakini hakutoboa.

“Nyamaza. Tangu nikuoe haujawahi kunifanyia madharau hadi dada yako alipoanza kuishi hapa,” alimfokea mkewe.

Kulingana na mdokezi jamaa hakutaka kusikia lolote kutoka kwa mkewe wakati huo.

“Toka hapa haraka ama niwafukuze nyote. Wanawake wamejaa nikiamua nitaoa mwingine hata kesho,” buda alitisha.

Aliendelea kurusha cheche za matusi bila kuhofia chochote.

“Wewe umeshindwa hata kuolewa. Unakuja hapa na tabia zako kumpotosha mke wangu,” alifoka na kumuonya vikali shemeji huku akiapa kumtimua iwapo hatabadilika.

“Iwapo utaendelea na tabia zako chafuchafu na mke wangu aendelee na madharau yake, nitakufuza,” akasisitiza.