Habari Mseto

Akothee ahimiza wanawake kuiga nyayo zake

January 16th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI na mfanyabiashara Esther Akoth almaarufu Akothee amehimiza wasichana wachanga kuthamini elimu, badala ya kukimbilia ndoa kabla hawajakata kiu cha masomo.

Kupitia chapisho kwenye kurasa zake rasmi za Facebook na Instagram, msanii huyo wa kibao tajika cha ‘Give it To Me’, amesema wanawake wengi waliofanikisha ndoa ni waliothamini umuhimu wa masomo.

Alitumia jukwaa hilo kushawishi wasichana ‘kubugia’ masomo, ambapo alipakia vyeti vyake vya Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE) na cha Chuo Kikuu.

aliwahimiza wale waliositisha masomo kuweza kurejea na kukamilisha baada ya kupakia vyeti vya masomo kwenye mitandao ya kijamii.

Akothee, 43, alifanya KCSE 2004 miaka kadha baada ya kuonja ndoa.

Alizoa alama ya C+, matokeo yaliyomwezesha kujiunga na Chuo Kikuu miaka tisa baadaye – akafuzu kwa Digrii.

“Katika ujana wangu niliacha shule bila kujali umuhimu wake. Niligura masomo nikiwa kidato cha pili na kuchagua ndoa iliyoonekana kuwa mwelekeo, lakini maisha yalikuwa na mpango tofauti,” Akothee alisimulia.

Kulingana na mwanamuziki huyu ambaye ni mama wa watoto watano, ndoa haikumwendea alivyodhania.

Ilikuwa na pandashuka zako, japo hakuwa amesahau kwamba anapaswa kukamilisha masomo.

Alielezea, “Majukumu ya familia yalinirejesha nyuma, niliwapa wanangu kipaumbele, ndungu na familia ambao walikuwa himizo kwangu”.

Licha ya matamanio yake, mahangaiko yalizidi kumwandama na kukosa fedha za kujifadhili kukata kiu cha masomo.

Anasema ndoto zake kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) 2007, behewa la Mombasa, zilizidi kudidimia.

Ukosefu wa fedha ulimlazimu kuahirisha malengo yake hadi 2013 ambapo mianya ya ufanisi ilifunguka.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Mt Kenya (MKU), ambapo licha ya hatua hiyo anasema nusra uraibu wake kupenda ‘sherehe’ na raha umteke nyara.

Akothee alifuzu mwaka uliopita, 2023 kwa Digrii ya Usimamizi wa Biashara (Business Management).

Kwenye chapisho lake lililosisimumua mashabiki wake mitandaoni hasa wanawake waliogura masomo, alifichua kwamba ameanza safari kutia mfukoni Shahada ya Uzamili.