Bambika

Akothee katika ziara ya hisia kali ‘nyumbani’ kwa kina Omosh

February 6th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MASHABIKI kwenye ukurasa wa mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee wamempongeza baada ya kutangaza atakuwa anaelekea nchini Uswizi mwezi ujao kuwatumbuiza mashabiki wake.

Inafahamika kuwa kwenye taifa hilo (Uswizi) ndipo alikuwa amempata mume wa tano Dennis ‘Omosh’ Schweizer na kufunga pingu za maisha naye Aprili, 2023.

Mwanamuziki huyo kwenye mitandao yake ya kijamii alipakia ujumbe na bango lililotangaza Machi 2, 2024, atakuwa anatumbuiza  mashabiki kwenye tamasha la Ramogi.

Akothee, 43, alieleza mashabiki wake, katika ziara hiyo wataandamana na meneja wake Nelly Oaks, ambaye amekuwa akishukiwa kuwa mpenzi wake tena baada ya kukatiza mahusiano yake na Omosh.

“Uswizi. Jinsi ninavyopenda ardhi hii. Ni vyema niwafahamishe mapema usiseme haukupata taarifa hii, nitakuja na Nelly Oaks wangu,” alipakia Akothee.

Jumbe za mashibiki zilianza kumiminika na kumsifia mama huyo wa watoto watano kujituma.

Shabiki Min Andy, alichangia kwa kumweleza mwanamuziki huyo kufanya kinachomfurahisha.

“Nakupenza binti, fanya kinachokufurahisha, ni nani anajali?” alisema Min Andy.

Hata hivyo kuna ujumbe mwingine uliokuwa na utatanishi, aliondika kwa lugha ya Dholuo.

Ujumbe huo ukidhihirisha mapenzi akimtaja mmoja wa rafiki yake.

“Nakupenda mpenzi, hivi karibuni nitakuona, Nakupenda zaidi (Ich liebe dich mein schatz, Bis bald, Beatrice Schnelli-Okello Ich liebe dich),” aliendelea Akothee.

Ujumbe huo ulichangamkiwa na mashabiki wengi.

“Kibwagizo kwenye sentensi hiyo, kimegonga ndipo…Hata hivyo tukisoma kwa dholuo inapendeza muno,” alisema Obanda Jaccodull.

Dan Ben Genga aimkosoa mwanamuziki huyo kwa kufichua atakuwa anaandamana na maneja wake kwenye ziara huyo.

“Hivi ni vita. Naomba upone kisha uendeleze penzi lako na Nelly Oaks. Usiwe mwepesi wa kutataizika na yaliyopita mkiwa na Mosh. Itakutatiza zaidi na vitu vingine vitaeta ugongwa hata kwenye usuhusiano wako na Nelly,” alisema Dan Ben Genga.

Hii itakuwa ziara ya kwanza kwa Akothee nchini Uswizi tangu alipoachana rasmi na aliyekuwa mume wake, Denis ‘Omosh’ Schweizer mwezi Julai. Mwanamuziki huyo na Omosh walikuwa wamepanga kufanya harusi ya pili nchini humo mnamo Julai, 2023 ila hilo halikutokea.

Akothee alithibitisha kuvunjika kwa ndoa yake na Omosh mnamo mwezi Novemba aliposhiriki kipindi cha moja kwa moja na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Katika kipindi hicho, alidokeza kuondoka kwenye ndoa hiyo baada ya kujifunza mambo kadhaa ambayo hakujua hapo awali.