Bambika

Akothee ni kielelezo kwangu licha ya tofauti za kifamilia – Cebbie Koks

February 4th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MSOMI Cebbie Koks Nyasego, ambaye ni dadake mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee, amethibitisha kuwepo kwa tofauti za kifamilia, lakini akisisitiza kuwa bado mapenzi kwa dadake yapo na hakuna anayeweza kubadilisha.

Kwenye mahojiano na Lynn Ngugi, Cebbie alishangazwa jinsi ambavyo watu mitandaoni hutuma jumbe za kumlaumu bila kujua kinachoendelea kwenye familia.

“Hili ni jambo ambalo ninataka kuzungumzia kwa uwazi. Yule ni dadangu wa toka nitoke. Nikizaliwa nilimpata. Kile ambacho hamfahamu ni kwamba dadangu ni rafiki wa chanda na pete,” akasema Cebbie.

Kwenye mahojiano hayo, Cebbie alimsifia dadake Akothee kwa yale mengi alimfanyia.

Pia, alisifu ukakamavu wake ambao umemwezesha kufaulu kwa mambo mengi maishani akiwa na umri wa miaka 30.

“…Amenilea kwenye safari yangu ya usichana. Unavyoniona inatokana na juhudi zake. Hisia za watu zaweza kuwa hisia zangu lakini haziwezi kutufafanua. Dadangu amefanya vizuri maishani mwake. Huyu ni mwanamke ambaye jamii ilitarajia aanguke chini zaidi,” akatiririka.

Binti huyo wenye umri wa miaka 32, alisema licha ya familia yake kuwa na misukosuko, anaamini siku moja atajaliwa kukutana naye na  kuwa na furaha kama hapo awali.

“Ni ombi langu kwa Mungu…. Nampenda na hadi wa leo nambari yake ya simu kwenye simu yangu nimeweka ‘Dada Mpendwa’, ni kipenzi kwa kila mtu… Iwapo kuna jambo mbaya laweza kutokea maishani mwangu, kwa uhakika atakuwa wa kwanza kufika kabla wewe,” alidhihirisha Cebbie.

Januari 24, 2024, katika video aliopakia mwanamuziki Akothee, alitangaza kwamba hatawa-miss nduguze kutokana na mambo waliyomfanyia mwaka 2022.

“Nilichoona kwa familia yangu Desemba 2022 nisingependa mtu yeyote apitie hilo,” alisimulia Akothee.

Kwenye simulizi hiyo alimaanisha hali yake ya kimawazo  alipokuwa kwenye uhusiano ambao uliisha.

“Nilikuwa katika mazingira magumu nilijihisi mpweke. Hiyo ndiyo hisia mbaya zaidi katika ulimwengu huu uliojaa watu. Hiyo ndiyo hisia mbaya zaidi ambayo mwanadamu yeyote anaweza kuwa nayo. Hasa baada ya kusaidia karibu kila mtu. Inaumiza,” aliongeza.