Al Duhail anayochezea ‘Engineer’ Olunga yarejelea mazoezi baada ya Kombe la Dunia kwa Klabu

Al Duhail anayochezea ‘Engineer’ Olunga yarejelea mazoezi baada ya Kombe la Dunia kwa Klabu

Na GEOFFREY ANENE

AL Duhail SC imerejelea mazoezi Jumatano baada ya siku mbili za mapumziko.

Klabu hiyo, ambayo imeajiri mshambuliaji Mkenya Michael ‘Engineer’ Olunga, ilikuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia kwa Klabu kutoka Februari 4-11 mjini Al Rayyan.

Ilimaliza ya tano baada ya kulima mabingwa wa Klabu Bingwa Asia Ulsan Hyundai kutoka Korea Kusini 3-1 katika mechi ya kutafuta nambari tano na sita (mwisho). Al Duhail ilikuwa imepoteza 1-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika na Misri Al Ahly katika robo-fainali.

Kocha Mfaransa Sabri Lamouchi alipatia vijana wake mapumziko ya saa 48.

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Qatar (QSL) 2019-2020 Al Duhail, ambao wanashikilia nafasi ya pili msimu huu wa 2020-2021, wataalika Al Rayyan ligini hapo Februari 14 uwanjani Abdullah bin Khalifa katika mchuano wa raundi ya 16.

Mnamo Jumatano, timu hiyo ilirejelea mazoezi. Ilianza na mazoezi ya viungo saa za asubuhi kwenye chumba cha kufanyia mazoezi kabla kuwa na kuingia uwanjani jioni kwa mazoezi zaidi.

Lamouchi anatarajiwa kuwa na kikao na wanahabari Alhamisi jioni kuzungumzia maandalizi ya mechi dhidi ya Al Rayyan. Al Sadd inaongoza jedwali kwa alama 41 ikifuatiwa na Al Duhail (28), Al Gharafa (27) na Al Rayyan (25) katika usanjari huo kwenye ligi hiyo ya timu 12.

You can share this post!

AKILIMALI: Lishe bora ya mifugo msimu wa kiangazi

Wachezaji wa Gor Mahia wagoma tena mechi ya CAF ikibisha