Habari

Al-Shabaab 10 wauawa na KDF Lamu

September 24th, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa Jeshi la Kenya (KDF) Jumatatu walifaulu kuwaua magaidi 10 wa kundi la Al-Shabaab na kujeruhi wengine kadhaa katika eneo la Taksile, kaskazini mwa Pandanguo, Kaunti ya Lamu.

Msemaji wa Jeshi la Kenya, Kanali Paul Njuguna alisema maafisa watatu wa KDF pia walijeruhiwa kwenye makabiliano hayo ya saa moja kasorobo asubuhi na tayari wamekimbizwa hospitalini wakipokea matibabu.

Bw Njuguna alisema KDF pia walinasa bunduki 7 aina ya AK-47, risasi na vifaa vingine vinavyotumiwa na Al-Shabaab kutekeleza mashambulizi eneo hilo.

Aliwataka wakazi kuwa macho na kupiga ripoti kwa walinda usalama iwapo watu wenye majeraha ya risasi watatokea kuwaomba msaada wa matibabu.

“Leo mwendo wa saa moja kasorobo, maafisa wetu walioko Lamu waliwashambulia Al-Shabaab na kufaulu kuwaua 10 ilhali wengine wakijeruhiwa vibaya. Wanajeshi wetu watatu pia walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo na wanapokea matibabu. Wakazi tushirikiane ili kumaliza magaidi hao na kuhakikisha usalama wa Lamu unadhibitiwa,” akasema Bw Njuguna katika ujumbe wake.

Kufuatia tukio hilo, msako mkali wa kuwatafuta magaidi waliotoroka na majetraha umeansishwa kwenye maeneo yote ya Taskile na Pandanguo nay ale yanayokaribiana na msitu wa Boni.

Mauaji ya Jumatatu ya Al-shabaab kumi yanajiri mwezi mmoja baada ya maafisa watano wa KDF kuuawa na wengine kumi kujeruhiwa vibaya kwenye shambulizi la kilipuzi cha kutegwa ardhini katika eneo la Sankuri kwenye barabara kuu ya Kiunga kuelekea Hindi, Lamu Mashariki.

Shambulizi hilo linaloaminika kupangwa na Al-shabaab lilitekelezwa Agosti 29.

Mnamo Agosti 8 mwaka huu, maafisa sita wa KDF saliuawa ilhali wengine watano wakijeruhiwa katika shambulizi sawai na hilo katika eneo la Kwa Omollo kwenye barabara ya Bodhei kuelekea Bar’goni.