Habari Mseto

Al Shabaab wajeruhi askari 9 

March 10th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MAAFISA tisa wa polisi wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa na wahalifu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabaab katika eneo la Dadaab, Kaunti ya Garissa.

Kulingana na taarifa kutoka Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) maafisa hao walivamiwa Jumamosi mwendo wa saa kumi na moja na nusu alfajiri (Machi 9, 2024) katika eneo la Welmerer walikokuwa wakiendesha doria ya usalama.

“Maafisa hao walikuwa wakisafiri kwa magari mawili kabla ya moja ya magari hayo kukanyaga kilipuzi cha kutegwa ardhi (IED) na kuharibiwa,” ikasema taarifa hiyo kuhusu kisa hicho kilichoripotiwa katika kituo cha polisi cha Hagadera na afisa wa cheo cha konstebo, Stephen Ndung’u.

Maafisa waliojeruhiwa katika shambulio hilo ni pamoja na; Samuel Mugo Muchina, Thaddeus Wabomba, Weldon Kipkoech Mutahi, Geoffrey Kangee, John Ngugi Njoroge, Gadsmile Chabari Kinyua, Franklyn Kweyu na Andrew Poghisio, wote wa cheo cha konstebo.

Mwingine aliyejeruhiwa ni afisa wa polisi wa akiba (NPR) Idle  Abdi Samoi.

Maafisa hao walipata majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao ikiwemo kichwa, shingo, vifua na mgongoni.

“Maafisa kutoka kitengo cha Kupambana na Magaidi (ATPU) katika eneo la Dadaab wanawaandama magaidi hao,” taarifa hiyo ikaeleza.