Alaba afunga bao na kusaidia Real Madrid kunyanyasa Barcelona kwenye El Clasico

Alaba afunga bao na kusaidia Real Madrid kunyanyasa Barcelona kwenye El Clasico

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipiga Barcelona 2-1 katika gozi kali la El Clasico lililowakutanisha uwanjani Camp Nou mnamo Jumapili.

Ushindi huo uliosajiliwa na masogora wa Real dhidi ya watani wao wa tangu jadi katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) ulifikisha alama zao kufikia sasa kuwa 20, tano zaidi kuliko Barcelona ambao chini ya kocha Ronald Koeman, sasa wanakamata nafasi ya tisa.

Gozi hilo la El Clasico lilikuwa la kwanza tangu 2004 bila aliyekuwa mvamizi wa Barcelona, Lionel Messi, na beki wa zamani wa Real, Sergio Ramos. Wawili hao walisajiliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa muhula huu bila ada yoyote.

David Alaba aliwafungia Real bao la kwanza katika dakika ya 32 kabla ya Lucas Vazquez kuongeza la pili katika dakika ya 90. Barcelona walifutiwa machozi na fowadi wa zamani wa Manchester City, Sergio Aguero sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Goli la Alaba lilitokana na mpira wa kushtukiza. Difenda huyo raia wa Austria aliyetokea Bayern Munich mwishoni mwa msimu uliopita wa 2020-21, alimpokonya Memphis Depay ndani ya kijisanduku cha Barcelona kabla ya kukimbia nao hadi upande wa pili kabla ya kushirikiana na Rodrygo kumwacha hoi kipa Marc-Andre ter Stegen.

Goli hilo lilikuwa lake la kwanza tangu ajiunge na Real na la kwanza katika gozi la El Clasico. Vazquez alikamilisha mpira aliorejeshewa na Ter Stegen aliyeshindwa kudhibiti kombora zito aliloelekezewa na Marco Asensio.

Bao la Aguero lilikuwa zao la ushirikiano wake na Sergino Dest na fataki yake hiyo ilikuwa ya pekee iliyoelekezwa na Barcelona langoni mwa Real katika kipindi cha pili na ikalenga shabaha.

Huku matokeo hayo yakiweka hai matumaini ya Real kutawazwa mabingwa wa La Liga kwa mara nyingine msimu huu, kocha Koeman anajipata katika presha ya kutimuliwa baada ya kikosi chake kutoridhisha mbele ya mashabiki 86,000 ugani Camp Nou.

Mkufunzi huyo raia wa Uholanzi aliwajibisha kikosi kichanga zaidi kilichojumuisha chipukizi Gavi, 17, aliyeweka historia ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuanzishwa kwenye gozi la El Clasico tangu 1941.

Koeman ndiye kocha wa pili wa Barcelona kuwahi kuzidiwa maarifa kwenye El Clasico mara tatu baada ya mkufunzi raia wa Ireland, Patrick O’Connell aliyepoteza mechi nne za kipute hicho kati ya 1935 na 1940.

Japo Real wanaotiwa makali na kocha Carlo Ancelotti hawakucheza kwa namna ya kuridhisha, waliibuka washindi nyumbani kwa wapinzani wao wakuu zaidi wa tangu jadi. Hakuna yeyote ambaye angewahi kudhani kwamba kikosi hiki cha sasa cha Real kingewahi kushinda Barcelona ya miaka 15 iliyopita.

Real kwa sasa wameshinda mechi nne mfululizo za El Clasico tangu watawale michuano saba mfululizo kwenye kivumbi hicho katika miaka ya 1960.

You can share this post!

Tielemans na Maddison wasaidia Leicester kuzamisha chombo...

Asingekuwa na mwito, mwenge wa uimbaji ungezima

T L