Habari Mseto

Aladwa ahimiza wanafunzi waliopata basari kutia bidii shuleni

April 14th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

MBUNGE wa Makadara, Bw George Aladwa amewataka wanafunzi ambao wamepigwa jeki ya basari kuongeza bidii maradufu na kufanya kazi kwa bidii katika taaluma zao na masomo kwa jumla.

Alisema hali hiyo inaweza kutoa uhalali sahihi wa kuendelea kutenga raslimali zaidi kwa minajili ya kufadhili elimu ya watoto kutoka familia zilizo na mahitaji.

Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa kugawa basari ya Sh30 milioni, Bw Aladwa aliwapatia hundi wanafunzi wa shule za sekondari, vyuo anuwai na vyuo vikuu katika shughuli iliyofanyika katika uga wa Camp Toyoyo.

Naibu kamishna kaunti ndogo ya Makadara, Bw Philip Koima na viongozi wengine wa eneo hilo walihudhuria na kuhutubia wakazi zaidi ya 3,000.

Bw Koima alitoa wito kwa wazazi, wanafunzi na viongozi wa mitaa kuunga mkono sera ya serikali ya asilimia mia moja ya mpito, kujiunga na shule ya upili.

Aidha, aliomba ushirikiano wa wadau ili kupambana na kero ya dawa za kulevya, pombe haramu na maovu mengine yote yanayosumbua jamii.

“Ninahimiza vijana kujiandikisha katika vyuo vya mafunzo ya kiufundi ili kupata ujuzi muhimu unaokidhi soko la ajira,” Bw Koima akasema.

Vilevile, Bw Aladwa alisema kamati ya pesa za ustawishaji maeneobunge Makadara (NG-CDF), ilizingatia usawa kutoka wadi zote nne ambazo ni; Kata za Viwandani, Harambee, Makongeni na Maringo/Hamza.

Bw Aladwa amewahi kuhudumu kama Meya katika jiji la Nairobi kabla ya katiba kubadilishwa.