Habari Mseto

Alai jela maisha akipatikana na hatia ya kusaidia Al Shabaab

July 2nd, 2019 2 min read

Na Richard Munguti

MWANABLOGU Robert Alai huenda akahukumiwa kifungo cha maisha akipatikana na hatia ya kuwasaidia magaidi wa Al Shabaab kwa kuchapisha picha za maafisa wa polisi waliokufa, katika mlipuko kaunti ya Wajir mnamo Juni 15, 2019.

Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi alimweleza Hakimu Mkuu Francis Andayi, kuwa kesi aliyoshtakiwa Alai ni mbaya na adhabu yake ni kali.

Alisema Bw Alai ameshtakiwa chini ya sheria mpya za kupambana na uhalifu zinazokabili visa vya ugaidi.

Bw Alai alikanusha mashtaka mawili ya kufanikisha visa vya ugaidi kwa kuchapisha picha za maafisa wanane wa polisi waliofariki katika kisa cha kulipuliwa na vilipuzi vilivyokuwa vimetegwa barabarani.

Alishtakiwa alichapisha picha hizo katika mtandao wake wa Twitter mnamo Juni 17 mwaka huu akijua polisi walikuwa wanachunguza kisa hicho.

Wakili Paul Muite aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema, “?hakuna makosa Alai alifanya ila kuwaarifu Wakenya jinsi polisi waliwasomba majeruhi kama magunia.”

Bw Muite aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana akisema ni haki yake. Pia alisema mshtakiwa alitiwa nguvuni Juni 17 na amekuwa kizuizini kwa muda huo wote.

Aliomba korti izingatie haki za mshtakiwa na kumwachilia kwa dhamana ya pesa taslimu.

Bw Alai aliachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu na kesi itasikizwa Agosti 8, 2019.

Maafisa wawili wa polisi, Safari Robert na Wilfred Kimaiyo, waliodaiwa kumsaidia Alai kupata picha za majeruhi hao, waliachiliwa na wanatarajiwa kuadhibiwa na idara ya polisi kwa utovu wa nidhamu.

Hakimu Mkazi, Bi Sinkiyian Tobiko alimwachilia Inspekta Kimaiyo kwa vile kiongozi wa mashtaka Angela Odhiambo alieleza korti kuwa hawatamfungulia mashtaka.

Akimwachilia Bw Kimaiyo, hakimu alisema, “afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) imefikia uamuzi hautafunguliwa mashtaka.”

Alisema hakuna sababu zozote zilizotolewa na DPP za kutomshtaki Bw Kimaiyo. “Hii mahakama haina budi ila kukuachilia kwa vile haina sababu za kuendelea kukuzuilia,” alisema Bi Tobiko.

Mahakama iliamuru afisa huyo mkuu wa polisi kutolewa pingu na kuachiliwa mara moja.

Watu wa familia ya afisa huyo wa usalama waliokuwa wamefurika kortini walipiga makofi na kushangilia huku wengine wakilia kwa furaha.

Alipofikishwa kortini wiki mbili zilizopita, hakimu aliombwa amwachilie inspekta huyo kwa dhamana huku akisifiwa kwa kutoa huduma kwa umma kwa miaka 20 kama afisa wa usalama.

Kiongozi wa mashtaka, aliieleza mahakama kuwa simu ya Insp Kimaiyo ndiyo ilikuwa inachunguzwa ili uhusiano baina yake na Bw Alai uweze kubainishwa, pamoja na magaidi hao wa Al Shabaab.

Hakimu aliombwa amwachilie Bw Kimaiyo ili akamuomboleze mwenzake aliyekufa katika shambulio hilo.

Bw Safari ambaye ni askari jela aliachiliwa pia bila kushtakiwa.