Makala

ALAINE NJOROGE: Ndoto yangu ni kuwa rubani

November 18th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WAHENGA waliposema kuwa dalili ya mvua ni mawingu kweli hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa. Katika masuala ya sanaa huaminika kuwa kwa baadhi ya wenye vigezo vya kubobea katika jukwaa hilo huonyesha dalili wakiwa wadogo pia huanza kama mzaha.

Alaine Wambui Njoroge ni msichana mdogo mwenye umri wa miaka 9, lakini anayofanya ni zaidi ya umri wake.

Alaine ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Braeburn Kawangware, Nairobi. Msichana huyu anasema tayari anahisi ana kipaji cha kutunga nyimbo maana anatamani sana kuibuka mwimbaji maarufu nchini na Afrika kwa jumla.

ALAINE VLOGS

Katika mpango mzima msichana huyu ana kipaji cha masuala ya sanaa ya uimbaji pia uigizaji. Kwenye jitihada za kuonyesha uwezo wake katika masuala ya sanaa pia kuwafikia wafuasi wake amefungua Chaneli yake katika jukwaa la You Tube inayokwenda kwa jina ”Princess Alaine Vlogs.’ Katika chaneli hiyo inaitumia kutupia kazi zake ikiwamo nyimbo, video fupi fupi za uigizaji pia video zake akiwahoji watu tofauti.

Katika mojawapo kati ya video zake alipata fursa kuwahoji waendeshaji pikipiki wawili kutoka Switzerland waliokuwa katika safari yaao kutembelea mataifa mbali mbali katika Kanda ya Afrika. Wawili hao walisema katika mpango wao wanatembea mataifa ya Afrika ikiwamo Kenya, Zambia, Namibia, Botswana, Afrika Kusini, Uganda, Rwanda na Tanzania.

INSPEKTA MWALA

Kwa mara ya kwanza wiki iliyopita msichana huyu alipata nafasi kushiriki cha uigizaji cha Inspekta Mwala ingawa bado kazi yake haijarushwa hewani. Chipukizi huyu alianza kujihusisha na masuala ya sanaa akiwa na umri wa miaka saba kipindi hicho akiwa mwanafunzi wa darasa la tatu. ”Binafsi sina budi kutaja kwamba ukuaji wa teknolojia umechangia wengi wetu kuwazia masuala ya sanaa,” msichana huyu alisema na kuongeza kwamba pia Shuleni huwa anashiriki masuala ya sanaa (drama).

Katika mpango mzima msichana huyu ana ndoto ya kuwa rubani kama taaluma yake pia kusaidia wengine kutimiza ndoto zao maishani. ”Kuhusu jinsi ninavyopanga ratiba yangu huwa nimepanga kila kitu na muda wake. Kuna wakati wa masomo pia kufanya vitu zangu za usanii maana pia ninalenga kufanya vizuri shuleni,” anafafanua.

Wakati wa mapumziko msichana huyu anapenda sana kutazama filamu iitwayo ‘The Worst Witch’ ya Marekani. Msichana huyo alizaliwa hapa Kenya na kulelewa katika jiji la Boston nchini Marekani. Katika michezo anasema anapenda sana uogeleaji. Kando na masuala ya sanaa kwa masomo anasema anapenda somo la Kiingereza na Sayansi.