Michezo

Alama tatu pekee Bayern itwae ushindi kwa mara ya 8 mfululizo

June 14th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich wanahitaji sasa alama tatu pekee kutokana na jumla ya mechi tatu zijazo ili kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa msimu wa nane mfululizo.

Hii ni baada ya masogora hao wa kocha Hansi Flick kuwakomoa Borussia Monchengladbach 2-1 katika mechi iliyowakutanisha uwanjani Allianz Arena mnamo Jumamosi usiku.

Leon Goretzka ndiye aliyewafungia Bayern bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwadumisha waajiri wake kileleni mwa jedwali kwa alama 73, saba zaidi kuliko Borussia Dortmund waliosalia katika nafasi ya pili baada ya kuwachabanga Dusseldorf 1-0. Goli la Dortmund lilipachikwa wavuni na chipukizi Erling Braut Haaland kunako dakika ya 90.

Bayern watatia kapuni ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya 30 katika historia mnamo Jumanne ijayo iwapo watawazidi maarifa Werder Bremen uwanjani Weser.

Tineja Joshua Zirkzee aliwaweka Bayern kifua mbele kunako dakika ya 26 kabla ya beki Benjamin Pavard kujifunga na kuwasawazishia wageni dakika 11 baadaye.

Ingawa bao hilo liliwarejesha M’gladbach mchezoni, hamasa yao haikutikisa uthabiti wa Bayern waliotawala kipindi cha pili na kuwazidi maarifa wapinzani wao katika takriban kila idara.

Licha ya kushindwa, M’gladbach wangali katika nafasi ya kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao japo huenda wakapitwa na Bayer Leverkusen ambao pia wanajivunia alama 56.

RB Leipzig waliowakung’uta Hoffenheim 2-0 wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 62, nne nyuma ya Dortmund waliochelewesha karamu ya Bayern kwa siku chache zaidi mnamo Jumamosi. M’gladbach wamesajili ushindi mara moja pekee kutokana na msururu wa michuano mitano iliyopita.

Vigogo Thomas Muller na Robert Lewandowski ambao kwa pamoja wamefungia Bayern jumla ya mabao 64 kufikia sasa msimu huu hawakuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Flick dhidi ya M’gladbach. Wawili hao walikuwa wakitumikia marufuku baada ya kuonyeshwa kadi za manjano katika mechi ya awali iliyowashuhudia wakiwapepeta Bayer Leverkusen 4-2 ugani Bay Arena.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumamosi):

Dusseldorf 0-1 Dortmund

Bayern 2-1 M’gladbach

Cologne 1-2 Union Berlin

Hertha Berlin1-4 Frankfurt

Paderborn 1-5 Bremen

Wolfsburg 2-2 Freiburg

Hoffenheim 0-2 Leipzig