Dondoo

Alazimika kutoa punda kama mahari

January 16th, 2020 1 min read

Na John Musyoki

SIAKAGO, Embu

JAMAA mmoja alilazimika kuwapa wakwe zake punda wawili ili kupunguza deni la kulipa mahari.

Inasemekana wazazi wa demu walikita kambi kwa polo wakidai walipwe mali iliyobakia.

Kulingana na mdokezi wetu, mwanamume huyo alikuwa akiahidi kulipa mahari lakini hakuwa akifanikiwa kupata pesa.

Majuzi, wazazi wa mkewe waliamua kwenda kupiga kambi kwake wakilalamika kwamba ameishi na binti yao kwa muda mrefu bila kuwapa chochote.

“Wewe, umepuuza kulipa mahari kwa muda mrefu. Umemtunga binti yangu mimba ya tatu na hujawahi kutulipa mahari licha ya ahadi nyingi.

“Hatuondoki hapa bila mahari na kama tutaondoka, hatutamuacha binti yetu,” mzee alimwambia jamaa kwa ukali.

Mjomba wa binti aliendelea kuwasha moto. “Msichana wetu alipotoka nyumbani hakuwa na mtoto. Sasa anajiandaa kupata wa tatu na haushughuliki kulipa mahari. Tutakuachia watoto wako uendelee kulea, sisi twende na binti yetu!” alifoka.

Jamaa alijaribu kuwaomba wakwe zake wampe muda zaidi ili atafute pesa, lakini walikataa katakata.

“Tupe chochote ulichonacho ama turudi na binti yetu,” baba ya demu alisisitiza.

Ilibidi kalameni awape wakwe punda wake wawili aliokuwa akiwategemea kubeba mizig nyumbani.

Inasemekana baada ya wageni hao kupewa punda walikubali shingo upande huku wakitisha kurejea tena kwa kalameni hivi karibuni, iwapo hataonyesha dalili za kumaliza kulipa mahari hiyo katika kipindi walichokubaliana.

Majirani walisema mwanamume huyo alikuwa akimpenda mkewe sana na vitisho vya wakwe havikumfurahisha kabisa, kwa sababu hakuwa na nia ya kutowalipa mahari.