Alenga kuwa Eluid Kipchoge wa usoni licha ya fani kuchangamsha na kuimarisha afya

Alenga kuwa Eluid Kipchoge wa usoni licha ya fani kuchangamsha na kuimarisha afya

Na PATRICK KILAVUKA

Michezo huchangamsha mhusika na kumpelekea pia kuimarisha afya mbali na kujigundua zaidi katika fani mbalimbali.

Hiyo ni kauli ya mwanariadha chipukizi Farida Wambui,16, mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Muthangari, Kaunti ya Nairobi analenga kufuata nyayo za Eluid Kipchoge katika riadha. Yeye ni mtoto wa tano miongoni mwa watoto saba wa Bw Chege Ali na Bi Chaulile Hellen.

Kiu, hamu na ghamu ya kuwa mtimkaji wa mbio ilianza kusakama akiwa darasa la nne. Wakati huo, alikuwa anapenda kutimuka mbio za mita 100 na za kupokezana kijiti za 4×400. Anasema mazoezi makali ambayo hufanya humjenga zaidi kuwa na maono ya kufika mbali kwani anaamini kwamba, kujinoa kunamwezesha kuwa mtimukaji wa kasi na kuwa na uwezo wa kuhimili dhoruba za ukimbiaji ukiwemo ugandaji wa misuli.

Anadokeza wakati mwingine hufanya mazoezi shuleni na wakati wa likizo, kujifua na Branice Ayiso ambaye amekuwa kichochezi chake kikuu katika kuyaweka malengo yake ya kuwa mkimbiaji mtajika. Hujinolea uwanjani Gatina wakati wa likizo.

Mwaka 2018, alishiriki katika mashindano ya michezo za Shule za Msingi yaliyoandaliwa Mombasa, kitengo cha riadha ambapo alikimbia katika mita 400 na 4×400 na kuwa miongoni mwa tano kabla kushiriki katika fainali za 2019 ambazo ziliandaliwa Kaunti ya Kakamega. Ana vyeti kadhaa vya kuvumisha riadha katika Kaunti ya Nairobi na kitaifa ambapo alikuwa wa kwanza katika kanda ya Nairobi mbio za 4×400 na kuwakilishi kitaifa.

Mwanariadha chipukizi Farida Wambui,16, akionyesha vyeti alivyotunukiwa katika ya mashindano ya Kanda ya Nairobi na kitaifa…Picha/PATRICK KILAVUKA

Anasema kwamba, nyanyake ni mwalimu wa michezo shuleni Susan Kimani pamoja na mkufunzi Njeri ndio wamempa motisha zaidi ya kukimbia wakimrai kwamba, akijitahidi sana katika kufanya mazoezi ya fani ya riadha, yaweza kumuinua na kuwa njia ya kipato kwake siku za majaliwa.

“Nyanyangu na walimu hufurahia na hunitia motisha sana kila wakati kuendelea kufanya mazoezi ili nijiongezee uwezo wa kuhimili dhoruba za ukimbiaji na jitihada zangu zimefua dafu na nimeyaona matunda,” alikariri mwanariadha huyo chipukizi ambaye ndoto yake ni kushiriki hata katika michezo ya Olympic siku moja majaliwa.

Ingawa ndwele ya Corona ilisitisha michezo ya shule na kuathiri mazoezi, amekuwa akifanya mazoezi ya kibnafsi kama njia ya kuendeleza azma yake ya kuwa mkimbiaji bora. Aidha, kupitia uchezaji wa kabumbu na timu ya Joylove Academy ambayo inashiriki Ligi ya Kanda ya Nairobi akicheza kama kiungo, chini ya kocha Joyce, anakiri kupata jukwaa la kujifanyia mazoezi ya ziada ya ukimbiaji.

Mwanariadha ambaye amesomba mawazo yake katika fani ya mbio ni mtimukaji mwenye kasi Eluid Kipchoge ambapo anasema hupenda kufuatilia masuala ya ukimbiaji wake akizoa maarifa jinsi ya kuwa mwanariadha wa kazi na kuweza kuhimili kizungumti cha ukimbiaji. Mbali na kuimarisha muda wa kutimuka.

Mwanariadha chipukizi Farida Wambui,16, aliye pia mwanasoka wa timu ya Joylove Academy,Nairobi akijinoa…Picha/PATRICK KILAVUKA

Changamoto yake ya fani hii ni kwamba, huwa wakati mwingine anahisi uchovu mwingi na misuli kuganda japo mazoezi huimarisha hali. Mwishowe anashauri kwamba, siri ya kuwa mtimukaji bora ni kufanya mazoezi tu na kuzingatia kanuni za kiafya.

You can share this post!

Bonyeza *106# kuthibitisha kama laini yako imesajiliwa...

Himizo amani idumu wakati wa uchaguzi

T L