Michezo

ALENGA REKODI: Kane ataka awe mfungaji bora wa muda wote 'Three Lions'

September 10th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza na aliyekuwa mvamizi wa zamani wa timu hiyo, Alan Shearer wamesisitiza kwamba fowadi Harry Kane ana kila sababu za kuweka historia ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa kikosi hicho.

Awali, Kane alikuwa amefichua kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake kila anaposhuka dimbani kuwajibikia Uingereza ni kuivunja rekodi ya mabao 53 inayoshikiliwa na aliyekuwa nahodha na kiungo mvamizi wa Manchester United, Wayne Rooney.

Mabao matatu yaliyofungwa na Kane dhidi ya Bulgaria katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Euro 2020 mwishoni mwa wiki jana yalimfanya kuifuta rekodi ya aliyekuwa nguli wa soka katika timu ya taifa ya Uingereza, Geoff Hurst.

Hadi sasa, Kane ambaye ni mshambuliaji matata wa Tottenham Hotspur anajivunia jumla ya mabao 25 kapuni mwake kutokana na mechi za kimataifa ndani ya jezi za kikosi cha Uingereza. Mabao yake yaliwezesha timu hiyo inayonolewa na Southgate kuzamisha Bulgaria 4-0 wikendi jana na hivyo kunusia tiketi ya kunogesha fainali za Euro mwakani.

Wingi wa mabao ya Kane kutokana na jumla ya mechi 40 pekee za kimataifa ni jambo linalomweka mbele ya Rooney.

Isitoshe, umri wake mdogo wa miaka 26 pekee unampa muda zaidi wa kufukuzia ufanisi wa kuvunja rekodi ya Rooney ambaye anatarajiwa kudhibiti mikoba ya Derby County nchini Uingereza mwishoni mwa msimu huu.

“Mabao ya Kane dhidi ya Bulgaria yalimwezesha kumpiku Hurst. Kwa sasa anasalia na magoli matano zaidi ili kuifikia rekodi yangu ya mabao 30. Ni suala la muda tu kabla aifute rekodi hiyo,” akatanguliza Shearer wakati wa mahojiano yake na wanahabari wikendi iliyopita.

“Kane atampiku Rooney na kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa timu ya taifa ya Uingereza. Umri wake unamruhusu na ana nafasi zote za kufanya hivyo kwa kuwa angali na miaka sita au saba zaidi ya kuchezea timu ya taifa,” akasema.

Mbali na wingi wa mechi za kirafiki ambazo kwa sasa Uingereza imepangiwa kushiriki hasa dhidi ya wapinzani wanyonge, Kane ana uwezo wa kupachika wavuni idadi kubwa zaidi ya mabao iwapo atashirikiana vilivyo na fowadi mahiri wa Manchester City, Raheem Sterling.

Kati ya mabao 25 ambayo Kane amewafungia Uingereza kufikia sasa, manane yametokana na mikwaju ya penalti.

Anatarajiwa leo Jumanne kuongoza safu ya mbele ya Uingereza watakaoshuka uwanjani St Mary’s kuchuana na Kosovo katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020.