Michezo

Alexis Sanchez na Ashley Young wasaidia Inter Milan kukandamiza Brescia

July 2nd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI Ashley Young, mshambuliaji Alexis Sanchez na kiungo Christian Eriksen walifunga bao kila mmoja na kuchangia mengine matatu katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyoshuhudia Inter Milan wakiwaponda wanyonge Brescia 6-0 uwanjani San Siro.

Young aliwaweka Inter kifua mbele kunako dakika ya tano baada ya kushirikiana vilivyo na Sanchez aliyefunga la pili kupitia penalti baada ya fowadi Victor Moses kuchezewa visivyo katika dakika ya 20.

Danilo D’Ambrosio alifungia Inter bao la tatu baada ya kujaza kimiani krosi ya Young katika dakika ya 45 kabla ya mpira wa ikabu uliochanjwa na Sanchez kufumwa wavuni na Roberto Gagliardini dakika saba baadaye.

Kombora la Romelu Lukaku ambalo lilipanguliwa na kipa wa Brescia lilirejeshwa langoni ma Eriksen katika dakika ya 83 sekunde chache kabla ya kiungo huyo mzawa wa Denmark kupakua krosi safi iliyokamilishwa na Antonio Candreva mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kipindi cha mkopo cha Sanchez kambini mwa Inter kilirefushwa hadi mwishoni mwa msimu huu na nyota huyo mzawa wa Chile anatazamiwa kurejea Manchester United wakati wowote kuanzia Agosti 2, 2020.

Chini ya kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte, Inter kwa sasa wanasalia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama nane zaidi nyuma ya viongozi Juventus wanaofukuzia ubingwa wao wa tisa mfululizo katika soka ya Italia.

Brescia wanavuta mkia kwa alama 18 na wapo katika hatari ya kuteremshwa ngazi kwa pamoja na Spal na Lecce.

MATOKEO YA SERIE A (Julai 1):

Inter Milan 6-0 Brescia

Bologna 1-1 Cagliari

Fiorentina 1-3 Sassuolo

Lecce 1-2 Sampdoria

Spal 2-2 AC Milan

Verona 3-2 Parma