Habari Mseto

Alfred Keter na wenzake wamtaka Uhuru kuhakikisha wakulima wamelipwa

October 4th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wanne wa Rift Valley sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati madhila ya wakulima wa mahindi kutokana na kucheleweshwa kwa malipo yao.

Wanasema hii ni baada ya kile wanachodai ni hatua ya mawaziri Henry Rotich (Fedha) na Mwangi Kiunjuri (Kilimo) kuwahadaa wakulima hao kuwa wangeanza kulipwa jumla ya Sh1.4 bilioni kuanzia Jumatatu kama malipo kwa mahindi waliowasilisha kwa maghala ya NCPB mwaka jana.

“Sasa tunamtaka Rais Kenyatta kuingilia kati suala hili kwani inaoneka mawaziri wake waliwahadaa wakulima. Japo walisema wakulima watapata pesa Jumatano lakini hadi sasa hakuna hata mmoja wao amelipwa,” mbunge wa Moiben Silas Tiren akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Alikuwa ameandamana na wenzake; Alfred Keter (Nandi Hills), Joshua Kandie (Baringo ya Kati) na Sammy Saroney (Mbunge Maalum).

“Tunafasiri kucheleweshwa kwa malipo ya wakulima kama njama ya kuwavunja moyo wakulima ili kutokana nafasi kwa watu fulani kuendelea kuagiza mahindi kutoka. Swali, ni je, mbona NCPB iliwalipa haraka wafanyabiashara na matapeli walioagiza mahindi kutoka Maxico, Brazil, Uganda na Tanzania ilhali wakulima halisi hawajalipwa mpaka sasa,?” akauliza Bw Tiren.

Wiki jana Waziri Rotich na Kiunjuri walisema Sh1.4 bilioni zingeanza kusambazwa kwa wakulima kuanzia Jumanne baada ya zoezi wa kuwakagua wakulima kukamilika.

Lakini kufikia Jumatano jioni wakulima waliohojiwa walisema hawajapokea pesa zozote katika akaunti zao.

“Inaonekana kuw mawaziri Rotich na Kiunjuri walikuwa wakituchezea shere maana mpaka sasa sijapata chochote,” akasema mkulima kutoka eneo la Soi Benjamin Rop.

Zaidi ya wakulima 800 walitarajiwa kufaidi kutokana na Sh1.4 bilioni ambazo serikali ilitoa, pesa zinazowakilisha asilimia 60 ya Sh3.5 bilioni ambazo wakulima wanadai serikali.

Wakati huo huo, Bw Keter alitoa makataa ya hadi Jumatatu juma lijalo kwa serikali kuwalipa wakulima la sivyo watawaongozwa wakulima wa mahindi katika maandamano ya kuilaani serikali.

“Ikiwa kufikia Jumatano juma lijalo serikali haitakua imetoa pesa za wakulima, tutaandaa maandamano makubwa katika miji yote iliyoko katika maeneo kunakokuzwa mahindi.”

“Tunataka kusimama na wakulima na hivyo tutahimiza kufanya maandamano katika barabara za miji ya Eldoret, Kitale, Moi’s Bridge, Kapsabet, Nakuru na hata Bungoma,” akasema Bw Keter ambaye ni mbunge mbishani.