ALI SHISIA: Kiswahili kama chombo cha umoja na maendeleo endelevu Afrika Mashariki

ALI SHISIA: Kiswahili kama chombo cha umoja na maendeleo endelevu Afrika Mashariki

NA ALI SHISIA

KUTAMBUA na kukienzi Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana Afrika hakuna budi kuungwa mkono kwa kushirikisha kikamilifu watu wa Afrika.

Uelewa wa jamii, uwajibikaji na juhudi za pamoja ni mambo muhimu sana katika kuendeleza Kiswahili na matumizi yake.

Kiswahili kimekuwa na kinaendelea kuwa zana muhimu katika mapambano ya ukombozi wa Afrika na katika kujenga umoja na maendeleo ya Afrika.

Kama lugha ya mawasiliano mapana Afrika tangu zama za ukoloni na lugha iliyotumika katika vuguvugu la Umajumui wa Afrika kupigania utambulisho na maendeleo ya Afrika, Kiswahili sasa kina majukumu mapya Afrika yanayokipa uhalali wa kuendelezwa kama lugha ya kimkakati na utangamano.

Juhudi za sasa za kuendeleza Kiswahili na matumizi yake ni matokeo ya hali halisi ya ndani na nje ya Afrika pamoja na utashi wa jamii mbalimbali za Afrika wa kutambua na kuendeleza Kiswahili kwa ushirikiano wa pamoja.

Baada ya kuanzishwa kwa sera za masoko huria, hali ya Afrika Mashariki imebadilika sana kutokana na mwamko na hamasa miongoni mwa wananchi wa kawaida kujitokeza kufanya shughuli nyingi za biashara.

Kwa sasa, mchango wa watu wa kawaida katika kuwafikia na kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki ni mkubwa mno ukilinganisha na ule wa serikali na kampuni za kitaifa au za kigeni.

Wananchi wa kawaida ambao ni wafanyabiashara ndio kiungo kikubwa kwa sasa baina ya wazalishaji na wananchi.

Maingiliano haya ambayo yameshika kasi yanaakisi hali halisi ya ushirikiano mpya wa Afrika Mashariki ulivyo na unavyoendelea kukua na kutekelezwa.

Maingiliano hayo sasa yanaibua suala la lugha ya kutumika katika kuwaunganisha na kuwashirikisha watu wengi zaidi na wa viwango tofauti vya elimu.

Si ajabu kuwaona au kukutana na raia wa mataifa mbalimbali humu nchini wakijishughulisha na ngange zenye kuwakwamua kutokana na umaskini.

Binafsi nimekutana na raia kutoka Burundi, Uganda, Demokrasia ya Kongo, Tanzania, Rwanda na kadhalika wakijishughulisha na ‘kazi za mkono’ kama vile kuchuuza vitu masokoni, mahotelini na kadhalika.

Utawasikia wakijaribu kuzungumza na wateja wao wakitumia Kiswahili kisichokuwa kizuri almuradi wapate matilaba yao.

Ushirikiano mpya wa Afrika Mashariki umefungua milango mingi ya ushirikiano katika nyanja za biashara, elimu, uchumi, kijamii na kisiasa.

Mikakati ya kubuni soko la pamoja la bidhaa za biashara baina ya nchi hizo, sarafu moja n.k inaendelea huku shughuli zenyewe zikiwa zimeanza kujitokeza waziwazi miongoni mwa raia.

Mazingira ya kuiunganisha jamii ya Afrika Mashariki kiuchumi, kisiasa na kijamii yananufaika zaidi kutokana na matumizi ya Kiswahili na yataboreka zaidi katika nchi hizi iwapo Kiswahili kitatiliwa maanani, kitumiwe kama lugha sambazi na kila nchi ikumbatie matumizi yake ipasavyo.

Raia hawa kutoka mataifa ya Afrika Mashariki watazungumza na kuelewana kwa Kiswahili kisha kuafiki malengo yao kwa njia rahisi.

Serikali za Kenya, Uganda na Tanzania zinatakiwa kuwekeza zaidi katika kupanua uelewa na matumizi ya Kiswahili katika kanda hii.

Hivyo basi, Kiswahili kinatambuliwa kama Lugha ya Mawasiliano mapana Afrika kwa ajili ya utambulisho, utangamano na maendeleo endelevu ya Afrika.

Isitoshe, pawepo himizo la maendeleo na matumizi ya Kiswahili kama chombo cha umoja na maendeleo endelevu ya Afrika zaidi ya kuhakikisha Kiswahili kinatambuliwa, kinaendelezwa, kinahimizwa na kutumika kama Lugha mojawapo ya kazi ya Umoja wa Afrika.

Kutoa mafunzo ya stadi za mawasiliano katika Kiswahili ili kuunganisha na kushirikisha kikamilifu Waafrika katika kujenga umoja na maendeleo endelevu ya Afrika; Kujenga uhusiano wa karibu baina ya Kiswahili, lugha nyingine za Kiafrika, na lugha za kikoloni zinazoendelea kutumika Afrika; Kuingiza Kiswahili katika mfumo wa elimu Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Matiang’i apuuza kilio cha Naibu Rais

Polisi wasaka walioua mtu kwenye baa

T L