Akili Mali

Aliacha kazi akaenda kukuza uyoga, sasa hatamani kuajiriwa tena

May 28th, 2024 3 min read

NA FRIDAH OKACHI

KILIMO cha uyoga kimekuwa na manufaa kwa baadhi ya vijana ambao wanakumbatia na kufanya hiyo kuwa kazi yao ya kila siku, wakiepuka kuajiriwa rasmi.

Verah Nkirote Mburugu, 35, mkazi wa Rimpa, Kiserian, Kaunti ya Kajiado, ni miongoni mwa vijana walioacha ajira rasmi na kuanzisha biashara zao wenyewe.

Bi Mburugu alielezea kuwa mwanzoni alikuwa ameajiriwa nchini Uganda katika kampuni moja ya mauzo, lakini baadaye aliamua kuanzisha biashara ya kuuza maziwa ya yogurt, ambayo haikuleta faida ya kutosha.

“Nina shahada ya mauzo. Nilipokuwa nje ya nchi, marafiki watatu na mimi tulianzisha biashara ya kuuza maziwa ya yogurt, lakini hatukupata faida. Tulifanya biashara hiyo kwa mwaka mmoja lakini tukaona hatupati faida. Tulikuwa tunasambaza, lakini tulipoangalia vitabu, hatukupata faida yoyote,” alisema Bi Mburugu.

Hali hiyo ilimfanya kutafuta ushauri kutoka kwa marafiki zake, ambao walimshauri kuanzisha kilimo cha uyoga nchini Uganda.

“Nilipata mafunzo kutoka kwa rafiki ambaye alinionea huruma na kuniambia kuwa kilimo cha uyoga kinaweza kuleta faida kubwa.

Kwa hali niliyokuwepo, nilihitaji pesa,” alieleza. Mwaka wa 2019, alianzisha kilimo hicho na akaona mapato mazuri, jambo lililomshawishi kuacha kazi yake ya mauzo.

Mwaka wa 2020, alipokea ruzuku kutoka kwa serikali iliyolenga kuwasaidia vijana wakati wa janga la COVID-19.

“Nilipofahamu kwamba nitapokea pesa hizo kwenye akaunti yangu ya benki, nilianza safari yangu kurudi nyumbani. Wiki moja baadaye, nilipokea ruzuku hiyo na nikaanza mradi huu wa uyoga,” alianza kusimulia.

Kilimo cha uyoga ni mmea ambao unahitaji kukuzwa mahali popote ambapo kuna fangasi.

Nyumba ya uyoga

Verah Nkirote Mburugu akionyesha maganda ya pamba ambayo hutumia kupandia mbegu za uyoga. PICHA | FRIDAH OKACHI

Bi Mburugu alianza kujenga nyumba ya kukuzia uyoga, ambayo haipati jua kali, na kuweka vifaa vinavyozuia joto kali ndani ya nyumba hiyo. Bi Mburugu alisema kuwa licha ya kutumia taka, uyoga huo unapaswa kupandwa kwenye maganda safi ambayo hupikwa kwa mvuke.

“Sisi hatutumii udongo kama wengine, badala yake tunatumia maganda ya pamba au mahindi. Tunapokusanya maganda hayo, tunayapika kwa mvuke. Kwenye chombo tunachotumia kuondoa uchafu huo, kuna maji chini, na katikati tunaweka maganda hayo,” alieleza Bi Mburugu.

Sehemu ya pili, yeye na wafanyakazi wake huchukua maganda hayo ambayo yanadhaniwa kuwa safi baada ya kupikwa kwa mvuke kwa zaidi ya saa sita na kuanza kuyaweka kwenye karatasi za plastiki.

Inaaminika kuwa kwenye karatasi ya plastiki, wakati wa kuweka fangasi za uyoga, fangasi hizo zinaweza kusambaa haraka licha ya kupewa sehemu ndogo ya kupata hewa.

“Mchakato wa mbegu za uyoga huchukua kati ya wiki mbili au tatu, ndipo tunapoona fangasi hizo zinasambaa kwenye karatasi ya plastiki kama inavyohitajika. Wakati huo, tunaweka kwenye rafu ili kuangalia jinsi uyoga unavyoendelea kukua,” aliongeza.

“Wakati tunapoona kwamba mbegu au fangasi zimesambaa kwenye karatasi kama inavyohitajika, huo ndio wakati muhimu tunapoanza kunyunyizia maji kidogo.”

Unyevunyevu

Kilimo hicho huhitaji maji kwa kiasi kidogo, hii ni kutokana na mmea huo ambao unahitaji unyevunyevu pekee ili kukua. Hii ikiwa ndio sababu kuu ya binti huyo kukosa kupanda nje ya shamba mbali kujenga nyumba ambayo imesalia kuwa shamba.

Uyoga huo ambao humea na kuwa tofauti. Bi Mburugu alisema wengi wa wateja wake hawapendi uyoga ambao unakaa kuwa mkubwa. Na ukubwa huo ukichangiwa na hewa kukosa kufikia uyoga ambao haupati mwanga.

“Hiki ni kilimo ambacho kinahitaji utaratibu wake. Mimea hii inakulia kwenye chumba hivyo nikumaanisha hewa haingi jinsi inavyohitajika. Iwapo nitasema nifungue sehemu ya juu ya mabati, basi nitaangamia. Uyoga hautaki jua,” alisema changamota anayopitia.

Maangamizo

Katika kilimo hicho alitaja kuwa baadhi ya maangamizo anayopata ni kutoka kwa konokono ambao hula uyoga huo.

“Tatizo kuu ni konokono. Ukiangalia hapa utaona hii sehemu imeliwa. Na huyu ni konokono. Ili kukambiliana naye, inanilazimu mimi na wafanyikazi wangu tuanze kumtafuta hadi tumpate. Hakuna mteja ambaye anataka kula uyoga uliokuliwa na konokono,” aliongeza.

Katika kilimo cha uyoga, lazima kuwe na mambo matatu ili kufaulu kwenye kilimo hicho. Kwanya ni kupata hewa safi, mwangaza ambao husambaza madini ya vitamin D na kiwango cha chini cha joto au kuwa kati ya 5-16. Iwapo uyoga utakosa mwangaza basi uyoga huo utakuwa mrefu kuita kuzidi.

Soko la uyoga nchini kwa wakulima hao, hulenga jamii ya Wahindi na Wazungu. Bi Mburugu amewataka jamii mbalimbali nchini kukumbatia ulaji wa uyoga ili soko hilo kuimarika.

“Nahimiza jamii zingine kula uyoga ili soko lenyewe liweze kukua. Hapa nauza kilo moja ya uyoga kwa Sh400. Iwapo una Sh100 basi utapata robo ya uyoga huo,” alisisistiza.

Amewataka vijana wengine kutoka kaunti mbalimbali kukihusisha na kilimo hicho kilicho na mapato mazuri kwa familia yake.

Alieleza kuwa kando na kuuza uyoga huo kwa zaidi ya kilo 15 kwa siku, pia anauza maganda ya pamba na mbegu ya uyoga kwa wakulima wengine.

“Nimempa mama jukumu la kusambaza uyoga huo kwenye maduka mbalimbali mjini Nairobi. Kila siku majira ya saa kumi wafanyakazi wangu huanza kupakia. Na ni kati ya kilo 15- 20 ambazo husambazwa,” alieleza.

Licha kuwa na wateja wachache nchini wanaonunua uyoga na kutumia pale nyumbani, binti huyo ana maono ya kuanza kusambaza nje ya nchi. Analenga kusambaza uyoga uliokaushwa.

“Natamani kufanya biashara na mataifa ya nje. Nilichogundua ni kuwa uyoga uliokaushwa unaweza kuchukua kipindi cha mwaka mmoja au miaka miwili kabla haujaharibika,” alikamilisha Bi Mburugu.