Makala

AKILIMALI: Alienda Mombasa kusaka ajira lakini akageuka mkulima mahiri wa ndizi

October 3rd, 2019 2 min read

Na HASSAN POJJO na LUDOVICK MBOGHOLI

HAMISI Bakari, 41, ni mzaliwa wa Matungu katika kijiji cha Namasanda huko Mumias, eneo la Magharibi mwa Kenya, aliyeajiriwa kazi ya kuuza vitambaa kwenye duka la Mhindi lililoko katikati mwa jiji la Mombasa.

Kwa sasa bwana Hamisi Bakari ni mkulima wa kujitegemea anayekuza zao la ndizi eneo la Chaani.

“Nilitoka kwetu nikiwa mkulima, nikaja Mombasa kuajiriwa. Lakini kazi niliyoipata ni ya kuuza vitambaa vya nguo na leso kwenye duka la Mhindi,” Bakari aambia Akilimali kwenye mahojiano.

Anasema alijitahidi sana.

“Kuuza kwa Mhindi kunahitaji moyo kwani nilishindwa kuendelea na kazi, ndipo nilipoamua kuanza shughuli za ukulima. Niliona ardhi ya Chaani hapa Changamwe ni yenye rutuba. Na kwa kuwa nilizoea ukulima huko nyumbani, nilihisi nianze rasmi kuitumia ardhi hii kwa kilimo,” Bakari afichua.

Anaongeza: “Ni sehemu ndogo sana niliyoianzishia ukulima kama hatua muhimu ya kunitoshelezea mahitaji ya kifamilia.”

Kulingana na mahojiano yake na Akilimali, uhaba wa mashamba mjini Mombasa haukumfanya akose kutimiza ndoto yake.

‘Nakubali hapa mjini kuna uhaba wa ardhi kwa ukulima, lakini haijalishi kwani uzoefu wangu umenipa maamuzi mapya ya kuwa mkulima stadi wa ndizi. Nilipania kuwa mkulima wa mashinani na hivyo badala ya kung’ang’ania kazi ya kuajiriwa, nikaanza kutafuta kazi mbadala ambayo ndiyo hii,” mkulima huyu adokezea zaidi Akilimali.

Hata hivyo Akilimali imegundua hamu kubwa ya Hamisi Bakari ni kujishugulisha na kilimo mseto, mbali na ukuzaji wa zao la ndizi.

Kama tulivyosema awali, Hamisi Bakari aliingia mjini Mombasa kutoka Mumias miaka 24 iliyopita, ambapo alitafuta kazi za kuajiriwa kabla ya kufanikiwa kazi kwenye duka moja linalomilikiwa na mfanyabiashara wa kihindi katika eneo la Mwembe kuku (biashara street).

Kazi aliyokuwa akiifanya ni kuuza vitambaa vya nguo na vipande vya Leso, lakini baadaye aliiona kazi hiyo haimfai, akaanza shughuli za ukulima wa mboga za kila sampuli sawa na ukuzaji wa zao la ndizi.

“Nilianza ukulima wa mboga za sukumawiki, mchicha, kunde na mabenda miongoni mwa mazao mengineyo,” asema Hamisi Bakari.

Anaendelea kutoa ufafanuzi.

“Hata hivyo sasa nashughulikia ukuzaji wa zao la ndizi, ambao nahisi unanikidhia mno mahitaji yangu. Hapa situmii mbolea maana udongo ni mzuri zaidi. Miongoni mwa sampuli za zao la ndizi ninazokuza zinatoka huko kwetu Mumias. Aina hizo ni mbokoya, shikhuthi, nashirembe na likomia (mkono wa tembo),” aarifu Akilimali.

Kutokana na juhudi zake tangu aanze shughuli za ukulima, tayari bwana Hamisi Bakari amenufaika pakubwa si haba.

‘Kwa kweli naona mafanikio makubwa mno kwenye shughuli hizi za ukulima. Miaka 4 iliyopita (mwaka wa 2015) nilianza kupata mafanikio makubwa ya ukulima, ndipo nilipoamua kuwa mkulima kamili kwa kuanzisha ukulima mseto’ asisitizia Akilimali.

‘Niliagiza aina tofauti za mbegu za ndizi (migomba) kutoka kwetu Mumias, nikazipanda na sasa naona mafanikio na faida yake’ asema mkulima huyu.

Aidha, Akilimali imegundua kuwa Bakari Hamisi ndiye mkulima wa pekee katika eneo ambalo anaishi.

‘Ni kweli, hapa ni mjini na hakuna wakulima. Mimi pekee ndiye niliyeamua kutumia ardhi hii kwa ukulima, hasa baada ya kugundua ina rutuba nyingi na muda mrefu imekuwa akikaa bure bila kutumiwa,” aelezea zaidi.

Kuhusu ushauri wake kwa wakazi wa Mombasa, mkulima Hamisi Bakari anasisitiza umuhimu wa kujituma kimaisha.

“Kama unaishi hapa Mombasa, usikae bure ukitafuta kazi ambazo hazipatikani. Kama hakuna kazi ya kufanya, tafuta kipande cha ardhi isiyotumika na uanze kushughulikia ukulima,” adai Bakari.

‘Wengi hudhania mjini hakufai kulimwa mazao, mbona mimi nimelima ndizi na najipatia faida?’ aliuliza mkulima huyu wa mjini.

Anadai maeneo ya mjini yana mapande ya ardhi yanayokaa bure ambayo yanaweza kutumiwa kwa ukulima.

‘Matajiri wanaomiliki ardhi kubwa ambazo hazitumiki, wawape wanaotaka kuzistawisha kwa ukulima ili wajipatie riziki. Sio vizuri ardhi hizo zikae miaka mingi na hazistawishwi’ ashauri bwana Hamisi Bakari kwenye mahojiano na Akilimali.