Makala

Aligura kazi ngumu ya kuuza mashamba akaanzisha kampuni ya uchukuzi, sasa ni tabasamu tu

June 25th, 2020 2 min read

NA PETER CHANGTOEK

LOISE Kamanu alikuwa ameajiriwa katika kampuni moja ya kuuza mashamba nchini kufanya shughuli ya uuzaji. Hata hivyo, kwa kuwa mshahara ambao alikuwa akiupokea ulikuwa mdogo sana, akaamua kuacha kazi hiyo, kusudi aianzishe kampuni yake.

Kwa wakati huu, yeye ni mmiliki wa kampuni ya usafirishaji wa bidhaa na mizigo, ijulikanayo kwa jina Modest Collections, iliyoko jijini Nairobi.

Mjasiriamali huyo alizaliwa katika eneo la Matasia, takribani kilomita tatu kutoka mjini Ngong, Kaunti ya Kajiado.

Baada ya kukamilisha masomo yake katika Shule ya msingi ya Greenyard, akajiunga na Shule ya Upili ya Serare – zote ziko katika Kaunti ya Kajiado.

Baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, ambapo alisomea shahada ya Ushauri wa Saikolojia (Counselling Psychology) na astashahada (certificate) katika Lugha ya Ishara.

“Mnamo mwaka 2015, niliajiriwa katika kampuni ya kuuza mashamba. Ilikuwa vigumu kupata mauzao………. nikaamua kuacha kazi na kujitosa katika biashara ya mitandaoni. Nilianzisha Modest Collections mwaka 2016 ili kuuza mabegi na bidhaa nyinginezo kwa kutumia majukwaa ya mitandao kama vile; Facebook na Instagram,” asimulia mjasiriamali huyo mwenye umri wa miaka 26.

Anafichua kwamba alianzisha biashara hiyo kwa kuutumia mtaji wa Sh20,000 alizopokea kutoka kwa familia na chama ambapo alikuwa mwanachama.

“Baada ya mwaka mmoja akiwa kwa biashara hiyo ya kuuza mabegi na bidhaa nyingine, nikahitaji hudumu za usafirishaji kutoka kwa stoo ambayo nilikuwa nimekodi kutoka kwa rafiki yangu. Mchakato wa kusambaza kwa wateja ukawa mgumu kwa sababu nilikuwa nikitumia bodaboda zozote na bidhaa zikawa zinafikishwa zikiwa zimechelewa au zikiwa zimeharibika,” aeleza Kamanu, ambaye ni mwasisi na afisa mtendaji wa kampuni hiyo.

“Hilo ndilo lililonifanya kuwa na wazo hilo; kama nilikuwa nikipata taabu kusafirisha bidhaa zangu, mwengine alikuwa akipitia changamoto pia,” asema, akiongeza kuwa alifanya utafiti na akagundua kuwa kwa kweli huduma za usafirishaji wa bidhaa zilikuwa zikihitajika sana.

Kamanu anafichua kuwa kutoka wakati huo, kampuni ya Modest Collections ikabadilika na kwa wakati huu hutoa huduma za kusafirisha bidhaa na vifurushi kwa wauzaji wa mitandaoni, jijini Nairobi.

Pia, anasema kuwa wanapania kujitosa katika shughuli ya usafirishaji wa mizigo mizito kwa wingi. “Tuna pikipiki, magari madogo na malori,” aongeza.

Anasema kuwa asilimia 80 ya wateja wake ni wauzaji ambao huziuza bidhaa zao mitandaoni, ilhali asilimia 20 ni mashirika mbalimbali.

Anaongeza kuwa kampuni yake ilituzwa tuzo mbili mwaka 2019 kutoka kwa kampuni ya Bizna Kenya katika kategoria ya biashara.

Kwa mujibu wa mjasiriamali huyo ni kuwa changamoto kuu ni ada za juu sana anazotozwa kufanya biashara. “Ni lazima tulipe serikali kuu na serikali ya kaunti ili kufanya biashara,” adokeza.

Anakiri kuwa biashara zimeathiriwa na gonjwa la korona, ambalo limekuwa tishio kuu ulimwenguni.

“Biashara ziko chini, lakini tunafanya kazi kwa zamu……Pia, tunahimiza wafanyabiashara kukumbatia biashara kwa majukwaa ya mitandaoni kwa sababu ni njia ya kuwafikia wateja kwa urahisi wakati huu,” ashauri.

Anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika biashara kuwa, ili biashara inawiri, sharti mtu awe na ari kwa sababu “biashara si ya watu wanaokufa moyo.”

“Uvumilivu huhitajika. Kumbuka kuwa Roma haikujengwa kwa siku moja,” ahimiza Kamanu.

Mjasiriamali yuyo huyo ana matumaini makubwa mno kwamba katika siku zijazo, kampuni ya Modest Collections, ambayo kwa sasa inapatikana katika eneo la Ngara, Nairobi, itawaajiri wafanyakazi wengi zaidi.