Dondoo

Alihepa aliponibebesha mimba, nifanyeje?

August 13th, 2024 1 min read

MAMBO shangazi? Nilikuwa na mpenzi kwa miaka mitatu. Nilipata mimba yake na alipojua akatoweka na kukatiza mawasiliano. Sasa ni mwaka mmoja tangu nijifungue na sijamsikia wala kumuona. Nifanyeje?

Mpenzi wako alitoweka kwa sababu hakuwa tayari kuwajibika. Usitarajie kwamba atajitokeza tena katika maisha yako. Sasa umejua hatari ya kumwamini mwanamume kiasi cha kubeba mimba yake kabla hajakuoa.

Tulipatana baa, nikahamia kwake lakini simpendi

Nina miaka 30. Nilikutana na mwanamke fulani katika baa na tukapendana. Nilihamia kwake na tumeishi pamoja kwa mwaka mmoja. Lakini nimegundua simpendi na nataka kumwacha. Nishauri.

Nahisi kuwa uhusiano wenu haukutokana na mapenzi, ulichochewa na ulevi. Sielewi pia ni kwa nini ulihamia kwake badala yake kuhamia kwako. Kama umegundua humpendi, mwambie hivyo kisha uondoke.

Nashindwa nitaoa nani kati ya wawili niwapendao

Nina uhusiano wa kimapenzi na wanawake wawili, nahisi wakati wangu wa kuoa umefika na nimechanganyikiwa. Ninahofia pia wakigundua wataniacha. Nishauri.

Wewe ni tapeli wa mapenzi. Huwezi kuwa na wapenzi wawili kwa wakati mmoja na ndiyo maana umejipata katika hali hiyo. Chagua mmoja utulie kwake kwani wakijua unawacheza watakutema.

Ndugu zangu wamepinga ndoa ya mpenzi aliye na umri mkubwa kuniliko

Nina miaka 27 naye mwanamke mpenzi wangu ana miaka 45. Nimempeleka kwa wazazi na wamemkubali. Lakini ndugu zangu wamemkataa sababu ya umri wake. Naomba ushauri wako.

Usihangaishe moyo wako kuhusu msimamo wa ndugu zako kwa sababu hawana haki yoyote katika maisha yako. Wewe ni mtu mzima na una haki ya kufanya maamuzi ya maisha yako. Wapuuze na uendelee na mipango yako.