Bambika

Alikiba: Wakenya kiboko yao, TZ ni waoga wa maandamano

Na SINDA MATIKO July 2nd, 2024 1 min read

NYOTA wa bongo flava Ali Kiba, kawavulia kofia Gen-Z na Wakenya kwa ujumla akiwataja kuwa wazalendo kuwaliko Watanzania.

Kiba ambaye anayo sehemu ya familia yake Kenya (watoto wake) na aliyekuwa mke wake Amina Khaleef, ni baadhi ya mastaa wa mataifa ya nje walioonyesha uungaji mkono wa maandamano ya Gen Z ambayo yamekuwa yakiendelea nchini kupinga uongozi mbaya na hali ngumu ya maisha.

Akigusia matukio yanayoendelea Kenya, wakati akihojiwa na wanahabari wa Tanzania kwenye hafla ya kuendelea kuitangaza kituo chake cha habari Crown FM na TV, Kiba aliwapa shavu Wakenya.

“Tunatofautiana sisi na Wakenya tena kwa umbali mkubwa sana. Tupo mbali kabisa, hatuwagusi na sidhani hata ipo siku tutawafikia kwenye upande wa uzalendo. Wale ni wazalendo kweli, sisi tukizungumza kwa maneno, wao wanafanya vitendo. Kwenye uzalendo hatuwagusi hata robo,” amesema King Kiba.