Dondoo

Alilia pasta amsaidie kutaliki mke

February 10th, 2020 1 min read

NA MWANDISHI WETU

MALAA, MACHAKOS

Kalameni wa hapa, alimshangaza pasta wa kanisa la mkewe alipomuomba amsaidie kumtaliki mkewe.

Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa amechoshwa na tabia za mkewe ya kumdharau kila mara.

Inadaiwa jamaa alikuwa amejaribu mbinu zote za kuachana na mkewe lakini hakufua dafu. Duru zinasema mwanadada alipokuwa akienda kanisani, jamaa aliamua kumfuata polepole. Kanisani, jamaa aliingia katika ofisi ya pasta na kumlilia.

“Mke wangu ni mshiriki wa kanisa lako. Nyumbani hanipi amani. Amekuwa akinipa presha sana kwa mambo anayonifanyia,” jamaa alieleza.

Pasta alinyamaza kumsikiliza polo. “Sina raha kabisa. Najuta kumuoa. Nimejaribu kumfukuza lakini siwezi. Naomba unisaidie kumtaliki,” polo alilia. Yasemekana kabla ya pasta kumjibu mkewe alijitoma ofisini na kumwagiza pasta kutomsikiliza mumewe.

“Usiamini maneno ya huyo mlevi. Wewe endelea na kazi yako, asikupotezee wakati,” kipusa alimrai pasta.

Inasemekana jamaa alianza kumfokea mkewe huku akitoboa siri zake zote.

“Huyu mwanamke kitandani hatuangaliani. Akiondoka asubuhi yeye hurudi jioni na hataki nimuulize. Nisaidie nimpe talaka,” polo aliomba. Kulingana na mdokezi, pasta alimuomba polo kurudi nyumbani ili wasuluhishe mgogoro baadaye.

“Tutakuja kusuluhisha hayo mambo baada ya ibada. Nenda ukatulie na usinywe pombe,” pasta alimrai jamaa. Inadaiwa polo aliamua kuondoka huku akiapa kutumia mbinu zote kumtimua mkewe. “Nimechoka na sitaki kumuona kwangu.

‘‘Madharau yake yamenichosha. Atafute mume mwingine,” jamaa alisema huku akiondoka ofisi ya pasta.

Inasemekana baada ya ibada pasta alielekea kwa jamaa akiandamana na wazee lakini hawakumpata.

Haikujulikana ikiwa jamaa alifaulu kumtaliki mkewe au la.