Habari za Kitaifa

Mwanamume aeleza korti jinsi mshtakiwa alivyomtandika kwa madai ya kumpachika mimba

May 14th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

KULIKUWA na kioja katika mahakama ya Eldoret mnamo Jumanne wakati mwanamume mmoja alibubujikwa na machozi akisimulia jinsi mpenziwe ambaye walikuwa wameachana naye, alivyomtandika kwa madai alimpa ujauzito.

Bw Mohammed Ali alimwambia Hakimu Mwandamizi Kesse Cherono kwamba mpenzi wake wa zamani, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu kimojawapo nchini, alimshushia kichapo kabla ya kuharibu runinga yake ya thamani ya Sh45,000.

Mshtakiwa ambaye anasomea Shahada ya Maswala ya Kijamii, alishtakiwa kwa kutekeleza shambulio la kudhuru mwili wa mlalamishi.

Hati ya mashtaka ilieleza kuwa kisa hicho kilitokea Machi 3, 2024, katika kituo cha kibiashara cha Kesses katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Kulikuwa na kizaazaa mahakamani wakati mlalamishi ambaye hujitafutia riziki kupitia kazi za mtandaoni, alitupiana cheche za maneno na mshtakiwa alipokuwa akifunguka kuhusu mapenzi yao ya siku za nyuma ambayo kwa sasa yamekuwa sumu.

Hakimu alitazama kwa mshangao jinsi wapenzi hao wa zamani walivyotupiana cheche za maneno baada ya penzi kuingia doa.

“Saa nne za usiku mnamo Machi 3, 2024, mshtakiwa na rafiki yake walivamia nyumba yangu wakidai kwamba alikuwa na ujauzito wangu ambao kwa ufahamu wangu nilijua kuwa ni uongo,” akasimulia Bw Ali.

Akijitetea, mshtakiwa alidai kuwa Bw Ali alimshambulia mara kadhaa na kuongeza kuwa katika usiku huo wa tukio, walitofautiana tu kuhusu suala la ujauzito mbele ya marafiki zake wawili wa kike.

Aidha aliiambia mahakama kuwa awali marafiki zake wawili wa kike walishuhudia tukio ambapo alivamiwa na mlalamishi na kusababisha majeraha mabaya mwilini mwake.

Mlalamishi aliambia mahakama kuwa yuko tayari kutoa kesi iwapo mshatkaiwa atagharimia hasara kwa kumlipa angalau Sh40,000.

Hakimu katika uamuzi wake alimtaka mshtakiwa ambaye aliachiliwa kwa dhamana ya Sh20,000 kurejea mahakamani Mei 23, 2024, kwa maelekezo zaidi kuhusu kesi hiyo.

Kuhusu suala la mimba, mshtakiwa alimwambia hakimu kwamba “niligundua sina ujauzito lakini wakati ule nilishuku mwanamume huyo alikuwa amenipachika mimba kabla ya kuniruka”.