Alipata tenda ya Sh1.3bn miezi 2 baada ya kusajili kampuni

Alipata tenda ya Sh1.3bn miezi 2 baada ya kusajili kampuni

Na SAMWEL OWINO

MFANYABIASHARA mmoja alishangaza wabunge baada ya kubainika kuwa kampuni yake ilipata tenda ya Sh1.3 bilioni ya kuuza vifaa vya matibabu wakati wa janga la corona miezi miwili tu baada ya kuisajili.

Bw James Cheluley alisajili kampuni ya Shop N Buy siku ya wapendanao Februari 14, 2020, na mnamo Aprili 29 mwaka huo, akafika katika ofisi za Mamlaka ya Kusambaza dawa na Vifaa vya Matibabu (Kemsa) na kukabidhiwa zabuni ya kuuza Vifaa vya Kujikinga Kiafya (PPE).

Jumatano, Bw Cheluley aliambia kamati ya bunge inayochunguza sakata ya mabilioni ya pesa katika Kemsa kuwa aliingia katika ofisi ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa mamlaka hiyo, Bw Jonah Manjari akiwa na barua ya kuomba auze PPE na siku iliyofuatia akakabidhiwa barua ya kuuza vifaa vya thamani ya Sh1.3 bilioni.

“Nilikuwa nimeandika barua tatu na zote zilikataliwa lakini Aprili 1 nilienda Kemsa nikiwa na barua ya kuomba kuuza PPE na nikapatiwa barua,” Bw Cheluley akasema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Abdulswamad Nassir alisema kwamba haiwezekani kampuni iliyokuwa na miezi miwili baada ya kusajiliwa kuingia katika ofisi za Kemsa na kukabidhiwa barua ya zabuni ya Sh1.3 bilioni saa 24 baadaye.

“Watu kama wewe huomba maombi tofauti na wengine kwa sababu huwezi kuingia katika ofisi za Kemsa na kutoka na zabuni ya zaidi ya Shilingi bilioni moja,” akasema Nassir.

Licha ya kushinikizwa na wabunge ataje wamiliki halisi wa kampuni hiyo, Bw Cheluley alikataa na kusisitiza kuwa anaimiliki binafsi na hakuna aliyemsaidia kupata zabuni hiyo.

“Nimelaumiwa kuwa nilishirikiana na wanasiasa maarufu ila hiyo ni kuninyanyasa. Nimeona ripoti kwamba Naibu Rais alinisaidia kwa kuwa tunatoka kabila moja. Naibu Rais hakunisaidia. Mimi ndiye mmiliki wa pekee wa kampuni hii,” alisema Cheluley.

“Tumekuwa tukifanya biashara hata kabla ya corona. Hata sasa ukiingia katika ofisi zetu, utaona PPE na vitanda vya hospitali. Ni sadfa tulifanya biashara na Kemsa,” alisema.

You can share this post!

Asilimia 24 ya Wakenya hatarini kufa njaa

Wadau walia utalii unaendelea kusambaratika nchini