Makala

Alipata Ukimwi akifanya kazi Juba, sasa anahamasisha umma kujitunza na kukabili ueneaji

February 27th, 2024 3 min read

NA PETER CHANGTOEK

MJA anapopimwa na kupatikana na virusi vya Ukimwi, aghalabu hukabiliwa na kiwewe asijue la kufanya.

Ndiyo hali iliyompata Susan Wairimu Metta alipopimwa na kubainika bayana kuwa na virusi.

Licha ya hali yake, yeye ni mwanamke jasiri, asiyehofu na hutangaza hali yake waziwazi bila wasiwasi wowote.

Amekuwa akihamasisha watu kuhusu ugonjwa hatari wa Ukimwi na virusi, kwa kutumia majukwaa tofauti tofauti, mathalani Facebook, Instagram na YouTube.

Wairimu, mwenye umri wa miaka 42, amehitimu, na ana cheti katika masuala ya ushauri kuhusu virusi vya Ukimwi. Aidha, alisomea masuala ya huduma kwa jamii, na akapata stashahada katika Usimamizi wa Biashara.

Anafichua kuwa, 2018, alipokuwa akifanyia kazi kampuni moja mjini Juba, Sudan Kusini, hakuwa akihisi vyema, ingawa pia alikuwa akibanwa na msongo wa mawazo kutokana na masuala yaliyokuwa yakihusiana na kazi.

“Nilipoteza uzani na nilikuwa nikiuguaugua kila mara. Hatimaye, kampuni ikafungwa na nikarudi nyumbani bila kazi; jambo lililoniongezea mawazo,” asimulia.

Anaongeza kuwa, ilipofika 2019, mwili wake ulikuwa umedhoofika ghaya ya kudhoofika, na akapoteza uzani wake kutoka kilo 108 hadi kilo 60.

“Nilipoteza kilo nyingi, nywele, nikapoteza hamu ya kula, na nilikuwa nikiendesha kila mara, kuganda kwa miguu, malaria ya mara kwa mara na nikapoteza uwezo wa kuona vizuri,” asema.

Akabaki gofu la mtu.

“Niliamua kuenda kupimwa na nikapatikana na virusi vya Ukimwi. Kwa kuwa nilikuwa nimeona watu wakiishi na virusi, nilijua nitaishi tu,” afichua Wairimu, akiongeza kuwa, alichokuwa akihofia tu ni endapo dawa zisingefanya kazi kwa mwili wake.

Anadokeza kuwa, alikuwa ameandamana na dada zake alipoenda kupimwa hospitalini. Baada ya kujua hali yake, akashindwa kabisa kuwaarifu wazazi wake, hadi akawa na ujasiri wa kufanya hivyo, mwaka mmoja baadaye.

Anafichua kuwa haikuwa rahisi kuvumilia hali hiyo. Katika usiku wa siku ya kupimwa, hakupata hata lepe la usingizi. Alilia.

Akawa anajiuliza maswali ya balagha; asipate jibu la maswali hayo.

‘Watu watanichukuliaje? Je, maisha yatakuwa sawa tena?’ Haya ni miongoni mwa maswali yaliyokuwa akilini mwake.

Wairimu anasema kuwa, mwili unapoathirika na virusi, mara kwa mara, mtu hukabiliwa na maradhi aina ainati, kwa sababu kinga ya mwili huathirika.

Pindi tu alipomwarifu rafiki yake mmoja, aliyekuwa akifanya kazi ya ususi katika eneo la Kitengela, taarifa hizo zilienea kasi mno, mithili ya majivu yaliyorushwa hewani.

Kupokea simu nyingi

“Nikaanza kupokea simu kutoka kwa watu, na wengine wakaja kuniona bila kuamini; wakidhani ni uwongo. Nilijipata nikiwajibu ‘Ndivyo hivyo’,” akaambia Taifa Leo Dijitali, akiongeza kuwa, baadhi ya marafiki waliasi urafiki waliokuwa nao, huku wengine wakibaki naye.

Wairimu anakumbuka fika siku moja alipokuwa kwenye matanuzi na wenzake, ambapo walimvuta kando mmoja wao, kusudi asizungumze naye kwa sababu ya hali yake. “Nilicheka tu. Bado hupitia unyanyapaa, lakini si sana,” aongeza Wairimu.

Unyanyapaa – kutengwa, ni mojawapo ya changamoto ambazo watu walio na virusi vya Ukimwi hupitia, na anasema kwamba, watu wanafaa kuondoa dhana kuwa virusi huua.

Kulingana na Wairimu ni kwamba, wale wanaotafuta kazi za kuwa yaya hubezwa na kubaguliwa, hata wanapoamua kuwa wazi na kufichua hali zao kiafya kwa wale wanaotaka kuwaajiri.

“Kujipenda, kujifahamisha na kujikubali ni muhimu sana kwa mtu anayeishi na virusi,” ashauri Wairimu.

Aidha, ni jambo aula kwa waathiriwa kutia pamba masikioni wasije wakakerwa na matamshi yanayotoka vinywani mwa wale wanaowasimanga walio na virusi.

Anadokeza kwamba, tangu atangaze hadharani hali yake, watu wamekuwa wakimtafuta ili awashauri.

“Mimi na baadhi ya marafiki wangu, tuliamua kutengeneza kundi la WhatsApp ambapo huzungumzia changamoto zetu na kushirikiana pamoja,” afichua.

Wairimu anashauri watu waende kupimwa ili kujua hali zao.

Anaongeza kwamba, mja akipimwa na apatikane akiwa na virusi, na kujikubali, ataishi maisha marefu kama kawaida, na kwamba mtu anapopimwa na apatikane akiwa sawa, hafai kubagua na kubeza walioathirika na virusi.

“Mtu yeyote anaweza kupata virusi; hata wewe uliyeketi kwa nyumba. Pia, uonyeshe mapenzi kwa watu; kile ambacho watu huhitaji ni kupendwa, si kuhukumiwa,” asema Wairimu.