Makala

Alitamani kuwa muunda bidhaa na marufuku ya mifuko ya plastiki ikamfaa

October 16th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na LAWRENCE ONGARO

TANGU utotoni hadi mwaka wa 2017 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Charles Kimani alikuwa akitamani kazi ya utengenezaji bidhaa.

Kwa hivyo, serikali ilipopiga marufuku utengenezaji, uuzaji na uagizaji wa mifuko ya plastiki kutoka nje, mnamo 2018 wazo lilimjia kijana huyu kwamba anaweza kuanzisha kazi ya utengenezaji mifuko ya karatasi ya khaki na kuuza.

Lakini kwa kuwa Kimani alikuwa mwanafunzi, tena kutoka familia masikini, hakuwa na pesa za mtaji za kumwezesha kuanza biashara hiyo. Alijaribu kuomba fedha kutoka kwa jamaa wake wengine lakini hakufua dafu.

Lakini alipokaribia kupoteza matumaini, aliamua kukopa Sh1,600 kutoka kwa M-Shwari, apu ya kukopesha fedha kwa njia ya simu ya mkono ambayo inaendeshwa na kampuni ya Safaricom kwa ushirikiano na benki ya NCBA.

“Nilitumia fedha hizo kununua kilo sita ya mabaki ya karatasi za khaki kutoka kampuni moja inayotengeza bidhaa za karatasi katika eneo la viwandani, Nairobi. Karatasi hizo zilinigharimu Sh600. Kisha nikanunua makasi na mililita 100 ya gundi; zote zikinigharimu Sh400. Vile vile, nilinunua vipande vya mbao ambayo hutumia kuipa mifuko umbo hitajika,” Kimani anasema

“Hapo ndipo nilipoanza kutengeza mifuko midogo ya kufunga bidhaa za duka kama vile sukari, mahindi, mchele miongoni mwa zingine. Wateja wangu wakuu walikuwa wenye maduka na wafanyabiashara wa vitafunio vijulikanavyo kama “popcorn” katika eneo la Ruiru Kimbo, Kiambu nilikokuwa nikiishi wakati huo,” anaongeza kijana huyu ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne anayesomea kozi ya Masuala ya Biashara na Teknolojia ya Habari (Businness Information Technology).

Mwanafunzi huyu mwenye umri wa miaka 31, anasema kadri maafisa wa polisi wakishirikiana na wale wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) walivyoendelea kutekeleza marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki ndivyo hitaji la mifuko yake ya khaki iliendelea kupanda.

“Niliendelea kujikaza japo nyakati zingine nilishindwa kutimiza mahitaji ya watega wangu kwa sababu sikuweza kutengeneza mifuko hiyo kwa wingi zaidi. Hata hivyo, nilikuwa na matumaini kuwa Mungu angeendelea kunifungulia milango ya fanaka,” Kimani anaeleza.

Changamoto nyingine ambayo alikumbana nayo mwanzoni ni kuweza kuwashawishi baadhi ya wateja wake, haswa wenye maduka makubwa, kwamba bidhaa zake zilikuwa zenye ubora hitajika.

“Lakini baada ya wateja hao kushawishika kuwa mifuko yangu ni bora sawa na mingine inayotangezwa na kampuni zenye majina makubwa mambo yaliendelea kuwa mazuri kwangu,” Kimani anaeleza.

Baada ya biashara yake kupanuka, mapema mwaka huu, alihamia kata ndogo la Witeithie katika eneo bunge la Juja na kukomboa nyumba kubwa ambako huendeshea kazi yake.

“Baada ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na karatasi hizi naweza kuchuma faidi ya Sh40,000 kutokana na karatasi ya thamani hii, baada ya kuondoa gharama zote. Hii ni baada ya kipindi cha majuma mawili wakati biashara ni nzuri,” Kimani anafafanua.

Amewaajiri wafanyakazi wawili, Wilson Munde na Keziah Mzame, ambao aliwafundisha kazi na sasa wanasaidiana kulisukuma gurudumu la biashara yake.