Habari Mseto

Aliyeambukiza mwanamke HIV kimakusudi aachiliwa kwa dhamana    

March 5th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAUME anayeshtakiwa kwa kuambukiza mwanamke ugonjwa hatari wa Ukimwi (HIV/AIDS) ameachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 huku polisi wakisubiri kumpeleka hospitali kutoa sampuli apimwe kubaini hali yake.

Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi alimwachilia mshukiwa huyo baada ya ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia kusema mshukiwa huyo ana familia.

Ameoa na ana watoto na makazi yake yanajulikana.

Licha ya afueni ya korti, mshtakiwa hajafaulu kulipa dhamana hiyo na angali anazuiliwa katika gereza la viwandani jijini Nairobi.

Mshtakiwa alikana kumuambukiza mwanamke huyo ugonjwa huo usio na tiba, kimakusudi.

Endapo atapatikana na hatia, adhabu ya shtaka hilo mkabili ni kifungo cha maisha.

Polisi wanasubiri mshtakiwa akilipa dhamana na kutoka nje wampeleke katika maabara ya serikali akapimwe damu kubaini hali yake.

Ombi la mshtakiwa atolewe damu liliwasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka.

“Naomba hii mahakama iamuru mshtakiwa atolewe sampuli za damu kupimwa hali yake ili afunguliwe mashtaka mengine,” Bw Gachoka alimsihi hakimu.

Bw Gachoka alieleza mahakama kwamba mshtakiwa anakabiliwa na shtaka kwamba akijua ni mhasiriwa wa HIV alifanya tendo la ndoa na mwanamke bila kondomu kwa lengo la kumwambukiza maradhi hayo hatari.

Mshtakiwa amekana kati ya Oktoba 5, 2022 na Juni 30, 2023 akijua anafanya makosa alishiriki tendo la ndoa na mwanamke bila kondomu ilhali anajua ni mhasiriwa wa Ukimwi.

Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka kwamba ripoti kutoka kwa Mwanakemia wa Serikali ni muhimu kubaini ikiwa mshtakiwa ana HIV au la.

Bw Ochoi alielezwa endapo mshtakiwa atapatikana na virusi vya Ukimwi basi mashtaka yatabadilishwa.

Mahakama ilielezwa adhabu ya makosa hayo ya kuambukiza Ukimwi kwa hiari ni kali kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kufungwa maisha gerezani.

Bw Gachoka alieleza mahakama huenda afisi ya DPP ikamfungulia mshtakiwa makosa mengine kulingana na ripoti ya Mwanakemia wa Serikali.

Awali, Bw Gachoka aliomba kesi hiyo isikizwe faraghani mlalamishi asitambulikane kwa umma.

Bw Ochoi alikubaliana na matamshi ya kiongozi wa mashtaka, wakili wa mshtakiwa na wakili anayemwakilisha mwanamke huyo kwamba, “haki za mlalamishi zinapaswa kuzingatiwa ili asifedheheke.”

Mahakama iliamuru mshtakiwa azuiliwe katika gereza la Viwandani hadi pale atakapolipa dhamana.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Kachero Eunice Nyaga alipinga mashtakiwa anyimwe dhamana kwa vile ilikuwa vigumu kumpata.

Bi Nyaga aliomba mahakama iamuru mshtakiwa azuiliwe gerezani hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Akimwachilia kwa dhamana, Bw Ochoi alisema dhamana ni haki ya kila mshtakiwa na “upande wa mashtaka haujawasilisha ushahidi wa kutosha mshtakiwa anyimwe dhamana.”