Habari Mseto

Aliyechimba kaburi lake mwenyewe ajiua

November 18th, 2019 1 min read

Na George Odiwuor

MWANAMUME wa umri wa miaka 50 alijitia kitanzi mwezi mmoja baada ya kuchimba kaburi atakamozikwa katika eneo la Rachuonyo Mashariki, Kaunti ya Homa Bay.

Inadaiwa Charles Moseti alijitoa uhai kijijini God Okombo, lokesheni ya Kasewe baada ya kuchimba kaburi ambamo atazikwa. Mwendazake anatoka kaunti jirani ya Nyamira na alikuwa akifanya kazi Homa Bay.

Moseti alikuwa akifanya kazi ya kulinda nyumba kijijini God Okombo. Wakazi walipigwa na mshtuko walipogundua maiti ya mwendazake ikining’inia kwenye paa ya nyumba aliyokuwa akilinda. Hata hivyo, mwendazake hakuacha ujumbe kuhusu sababu yake ya kujitia kitanzi.

“Hajawahi kugombana na yeyote. Hakuwa ameonyesha dalili zozote kwamba angejiua,” akasema mkazi wa eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Mashariki, Charles Barasa alisema kuwa Moseti alikuwa amejichimbia kaburi lake.

Alisema, Moseti alitaka azikwe kwenye kaburi hilo baada ya kifo chake.

“Kiongozi wa kanisa alituambia kuwa mwendazake alichimba kaburi lake katika Kaunti ya Nyamira na kufanya mipango ya mazishi. Alichimba kaburi hilo mwezi uliopita,” akasema Bw Barasa.

“Hakuacha ujumbe wowote wa kuelezea sababu yake ya kujitoa uhai. Inaonekana alijitia kitanzi kwa sababu zake za kibinafsi. Hata hivyo, tunaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha maafa hayo,” aliongeza.

Maiti imehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya wilaya ya Rachuonyo Kusini mjini Oyugis ambapo inasubiri kufanyiwa upasuaji.