Habari Mseto

Aliyechoma mwili wa mpenziwe motoni

October 17th, 2020 1 min read

NA FRANCIS MUREITHI

Mwanamume wa miaka 34 aliyemdunga kisu kifuani mpenziwe wa miaka 23 na kuuchoma mwili wake amekamatwa Likia, Kaunti Ndogo ya Njoro kaunti ya Nakuru.

Kulingana na kamanda wa polisi wa Njoro Muganda Kisaka mwathiriwa huyo alitambulika kuwa Mercy Njeri Mbatia. Kulingana na ripoti ya polisi kisa hicho kilifanyika Oktoba 13 lakini mshukiwa huyo akaenda mafichoni.

Bw Kisaka alisema kwamba mshukiwa huyo alikuwa amechomwa kichwani, mikononi na miguuni. Mwili wa mwathiriwa huyo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha chuo kikuu cha Egerton.

“Baada ya kutenda kitendo hicho mshukiwa huyo alienda mafichoni lakini polisi walimkamata eneo la Mathangatua ,Likia Ijumaa,” alisema mkuu huyo wa polisi.

Kulingana na uchunguzi wa polisi wawili hao walikuwa wapenzi na wakatengana.

“Inaonekana kwamba mwanamume huyo alikuwa na wivu baada ya kutengana na msichana huyo na kuamua kumuua baada ya kukosa kurudiana,” alisema polisi.

Mkuu wa polisi alisema mshukiwa huyo anazuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Njoro na kesi lake linashungulikiwa na DCI. “Mshukiwa huyo atafikishwa kortini  Jumatatu na kushtakiwa kwa mauaji,”alisema Bw Kisaka.