Habari Mseto

Aliyedai kunyang'anywa shamba la ekari 100 na Ruto afariki

October 28th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWANAMUME ambaye alimshtaki Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kumnyang’anya shamba lake wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 aliaga dunia Jumanne.

Adrian Gilbert Muteshi alifariki akiwa na umri wa miaka 86, kulingana na chapisho la tangazo la kifo lililokuwa kwenye gazeti la Daily Nation.

Hata hivyo, familia yake haikutaja kilichosababisha kifo cha Bw Muteshi ambaye alifanya kazi na shirika la ndege la zamani la East African Airways.

Mnamo Juni 2013, korti ilimuamuru Dkt Ruto amlipe marehemu Sh5 milioni kwa kupanga njama ya kumpokonya shamba lake la ekari 100 katika Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa ghasia hizo zilizomsababisha Bw Muteshi kutorokea usalama wake.

Mahakama Kuu ya Nairobi kupitia Jaji Rose Ougo ilitoa uamuzi kuwa Bw Muteshi alithibitisha kwamba ardhi hiyo ilikuwa yake na alikuwa amepokonywa kwa njia isiyofaa na Dkt Ruto.

Akijitetea kortini, Dkt Ruto ambaye pia wakati huo alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki jijini Hague, alisema kuwa alinunua ardhi hiyo kutoka kwa watu aliowaamini walikuwa wakiimiliki.

Ingawa Naibu Rais alihiari kuondoka kwenye ardhi hiyo, Bw Muteshi alishawishi mahakama kwamba alifaa kulipwa fidia na gharama za kesi kwa muda ambao ardhi hiyo ilitwaliwa ndipo akatunukiwa Sh5 milioni.

Mfanyabiashara Hosea Ruto ambaye alihusika katika kumuuzia Naibu Rais ardhi hiyo ndiye alitoa ushahidi kortini kwa niaba ya Dkt Ruto.