Habari Mseto

Aliyedai Uhuru atafariki Machi 20 aagizwa kupimwa akili

March 12th, 2019 1 min read

Na MAUREEN KAKAH

MWANAUME aliyedai kuonyeshwa ndotoni na Roho Mtakatifu kuwa Rais Uhuru Kenyatta, apaswa kumuona kabla ya Jumamosi ili asipatwe na mkosi, atapimwa akili.

Mahakama ya Nairobi Jumatatu iliamuru kuwa Wilson Mwangi Macharia akapimwe akili kabla ya kutoa mwelekeo wa kesi hiyo.

Hakimu Zainab AbdulRahman, alisema mshtakiwa huenda akawa hana akili timamu, na kwamba ni uchunguzi wa daktari utakaotoa shaka hiyo.

“Mshtakiwa afaa kuchunguzwa kisha ripoti yake iwasilishwe mbele ya korti hii,” akasema.

Macharia ambaye ni mpiga rangi viatu anayeishi mtaani Kayole, Nairobi, aliambia mahakama kuwa Rais Kenyatta afaa kumuona ifikapo Machi 16, la sivyo afe baada ya siku nne.

“Mimi si mgonjwa. Roho Mtakatifu alizungumza nami. Bw Kenyatta atakufa iwapo hatanipigia simu ifikapo Machi 16. Mimi na Mungu wangu tutamwacha peke yake,” akasimulia mahakama alipopewa nafasi ya kufafanua madai yake.

Kesi hiyo itatajwa Machi 18, 2019.