Dondoo

Aliyedhani kaangukia mume aambiwa nenda kacheze huko

June 7th, 2024 1 min read

NA JANET KAVUNGA

MALINDI MJINI

MIPANGO ya mwanadada wa hapa ya kuolewa na kuanza familia ilitumbukia nyongo mpenzi wake alipomwambia kwamba hajawahi kuwazia kumuoa.

Kwa miaka mitatu, demu alidhani alikuwa amepata mwanamume wa ndoto yake ambaye wangeoana na kuanza familia.

Alikuwa amewapuuza wanaume wengine waliokuwa wakimrushia mistari ya mapenzi kwa kuwa alikuwa ameamini jamaa angemuoa.

Baada ya kusubiri jamaa ampose bila mafanikio, aliamua kumuuliza mipango yake kuhusu ndoa na akapata jibu lililomgonga kama bomu.

“Sijawahi kuwazia ukiwa mke wangu… wetu umekuwa uhusiano wa kuburudishana tu, samahani,” jamaa alimwambia demu na kuondoka bila kujali maumivu ambayo alimsababishia.