Kimataifa

Aliyedhaniwa kuwa maiti achomwa akiwa usingizini mochari

May 2nd, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

Beaumont, Texas

MFANYAKAZI wa mochari moja nchini Marekani alifariki baada ya kuteketezwa kimakosa na wafanyakazi wenzake wakidhani ni maiti, alipokuwa amelala.

Idara ya polisi wa Beaumont ilisema kuwa Henri Paul, wa miaka 48 alikuwa amelala katika gari ambalo huwa anatumia kubebea maiti baada ya kufanya kazi kwa saa 16 bila kupumzika.

Hata hivyo, wakati alipokuwa akilala, mfanyakazi mwingine alidhani kuwa ni maiti ya mwanamume wa miaka 52 aliyekuwa ameaga dunia katika ajali ya barabarani na akamsafirisha hadi sehemu ambapo maiti huchomewa.

Kabla ya mtu yeyote kugundua makosa hayo, tayari Henri alikuwa amechomwa kwa joto la digrii 1400 hadi 1800 na kusalia jivu.

Mfanyakazi mwenza Jenna Davis alisema alimsikia akipiga nduru kwa sekunde kama 15, baada ya sehemu hiyo ya kuchoma maiti kuwashwa.

“Mwanzoni hakujua mahali nduru zilikuwa zikitoka. Wakati tuligundua kilichokuwa kikiendelea, tayari muda ulikuwa umeisha. Tulizima mashine ya kuchoma lakini tayari alikuwa amekufa,” akasema Davis.

Davis alisema mfanyakazi aliyefanya kosa hilo ni mgeni na alikuwa amesahau kukagua kifaa kinachowekwa katika maiti ili kuzitambua, ndipo ajue alikuwa akiteketeza maiti inayofaa.

Alisema alisikia marehemu akipiga mayowe kwa uchungu wakati mashine hizo zilikuwa zikimteketeza kuwa jivu.

Polisi walianzisha uchunguzi kubaini matukio haswa ambayo yanazingira kifo cha mfanyakazi huyo.

Wachunguzi wamesema huenda wakamfungulia mfanyakazi aliyefanya hivyo mashtaka ya utepetevu wa kijinai.