Kimataifa

Aliyedungwa kisu atoka hospitalini kikiwa mwilini kutafuta sigara

February 27th, 2019 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

KAZAN, RUSSIA

MWANAMUME aliyekuwa amedungwa kisu mgongoni na aliyekuwa akielekea kufa alishangaza wahudumu wa hospitali moja, alipoanza kuondoka hospitalini kisu kikiwa mgongoni kwenda kutafuta sigara.

Mgonjwa huyo kwa jina Vladmir, 34, alihisi hamu ya kuvuta sigara ndipo akakosa subira na badala ya kusubiri atibiwe kwanza akaamua kuitafuta kisu kikiwa mgongoni.

Iliwalazimu wahudumu wa afya katika hospitali hiyo kumshauri arejee wodi, alipoambiwa kuwa alikuwa akielekea kufa.

Mwanamume huyo hakuwa na mavazi wakati wa tukio hilo kwani alikuwa na nguo ya ndani pekee, huku akijikokota akiwa ameinama, nacho kisu kikichomoza mgongoni.

Iliripotiwa kuwa alijeruhiwa walipokuwa wakipigana baada ya kulewa, japo hakukuwa na habari zaidi.

Kisu chote kilikuwa kimedungwa mwilini kupitia sehemu ya mgongo, sehemu iliyoonekana ikiwa ile ya kushika tu.

Aanza kutembea

Wahudumu wa afya hospitalini humo walikuwa wakihudumia kidonda chake, kisu kikiwa mwilini bado, wakati aliwaambia kuwa alikuwa na kitu cha kufanya na akaanza kutembea.

Alipoulizwa alipokuwa akienda, aliwajibu wahudumu wa afya “Kuvuta sigara.”

Licha ya kuwa uchi, kulikuwa na baridi kali na wahudumu walimwonya kwenda nje katika hali hiyo, wakimwambia “kijana utakufa sasa.”

Baadaye alidaiwa kufanyiwa upasuaji wa kutoa kisu hicho mwilini.