Aliyefutwa kwa kuugua afidiwa laki 2

Aliyefutwa kwa kuugua afidiwa laki 2

NA BRIAN OCHARO

MWANAMUME aliyemshutumu mwajiri wake kwa kumfukuza kazi kutokana na maumivu ya mgongo aliyopata baada ya kutumia pikipiki kwa muda mrefu ametunukiwa zaidi ya Sh200,000.

Mahakama ya Ajira katika eneo la Malindi ilimtunuku Emmanuel Limo Chang’oka pesa hizo baada ya kupata kwamba Plan International Kenya ilimfuta kazi kinyume na sheria.

Jaji Bernard Manani alisema ingawa kuachishwa kazi kwake kuliweza kuwa kwa nia njema, shirika hilo ilishindwa kutoa ushahidi wa kutosha kuunga mkono uamuzi huo.

“Aidha, kuna ushahidi utaratibu uliotumika kupunguza watu ulikuwa na mapungufu makubwa. Kwa hiyo, hatua ya mshtakiwa kumfuta kazi mlalamishi si ya haki,” alisema jaji huyo.

Bw Limo alituzwa Sh783, 984, lakini kwa sababu alikuwa amelipwa kiasi cha Sh490,039, shirika litamlipa zilizosalia kwa sababu hakuna ushahidi kuwa shirika hilo lilikabiliwa na changamoto ya kifedha ili kuhalalisha kutimuliwa kwa wafanyikazi wake, na kwamba mchakato uliotumiwa kutambua wanaopaswa kufutwa kazi haukuwa wazi.

Bw Limo aliajiriwa kama afisa wa ufadhili katika shirika linaloendeleza haki za watoto na usawa kwa wasichana.

Kazi yake ilihusisha mawasiliano ya jamii kwa watoto chini ya uangalizi wa Plan International Kenya.

Kutokana na hali ya kazi yake, alitakiwa kusafiri mara kwa mara kutoka ofisini kwake hadi shambani kukutana na watoto hao.

Shirika lilimpa pikipiki ili kuwezesha harakati hii.

Lakini hakufahamu kuwa huo ungekuwa mwanzo wa vita vyake na maumivu ya mgongo.

Baada ya kutumia pikipiki kwa muda, alipata matatizo katika mgongo yanayohusiana na matumizi yake ya muda mrefu.

Alisema alipotoa taarifa kwa uongozi wa shirika hilo kuhusu hali yake ya kiafya, alidai haikuchukuliwa vyema.

“Badala ya kutafuta njia mbadala za kuhakikisha kwamba niliweza kutekeleza kazi yangu kwa usalama, wasimamizi walianza kutafuta vijisababu vya kuniondoa,” alisema katika karatasi yake ya mahakama.

Aidha anadai kuwa kutokana na changamoto yake mpya ya kiafya, shirika hilo lilibuni mpango wa kusitisha ajira yake kwa kisingizio cha uziada.

Bw Limo alifutwa mnamo Novemba 2020 wakati Covid-19 ilikuwa ikiangamiza Wakenya na dunia nzima.

“Kwa maoni yangu, shirika hilo halikuwa na sababu za kusitisha mkataba wangu kwa sababu za uziada,” alisema.

Kwa upande wake, shirika hilo lilishikilia kuwa Bw Limo aliachishwa kazi kihalali kwa misingi ya uziada.

Ilidai kuwa ilichukua hatua hiyo kutokana na changamoto za fedha kwani gharama ya kuendesha programu zake ilizidi bajeti yake.

“Hii ililazimu shirika kufanya ukaguzi ulioonyesha kuwa lina wafanyakazi wengi na halina fedha za kutosha, na hivyo kuzorotesha utekelezaji wa majukumu yake ya msingi,” lilisema.

Kutokana na hali hiyo, shirika hilo lilieleza kuwa lililazimika kufanya marekebisho ya aina fulani, ambayo yalimaanisha kuwa baadhi ya wafanyikazi wake wangeachishwa kazi na baadhi ya nafasi katika shirika hilo kufutiliwa mbali.

  • Tags

You can share this post!

Uchafuzi wa mazingira huua watu 9m – Ripoti

TAHARIRI: Kongole kwa mashujaa wetu waliofana Brazil

T L